Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Bw. Albert Msovela amewataka viongozi na watendaji kuzingatia suala la uadilifu katika utendaji wa shughuli za Umma ili kuepukana na madhara yanayotokana na mgongano wa maslahi.
Akifungua mafunzo ya sheria ya maadili ya utendaji katika utumishi wa Umma na namna bora ya kujiepusha na mgongano wa maslahi kwa Viongozi na Watendaji wa Mkoa wa Shinyanga, yaliyofanyika jana tarehe 10/01/2020 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Msovela amesema kuwa, ana imani kubwa baada ya mafunzo hayo yenye lengo la kukumbushana kuzingatia Sheria, taratibu na kanuni, washiriki watasimamia vema kwenye maeneo yao ya kazi.
"Hivyo mafunzo haya yanasisitiza katika kutekeleza majukumu yetu kusimamia sheria za Nchi, haki na utu ili kumsaidia mhe. Rais katika kutekeleza majukumu yake na hatimaye kutoa huduma bora kwa jamii" amesema Msovela.
Amesema kuwa tofauti na miaka ya nyuma, suala la mgongano wa maslahi limepungua kwa kiasi kikubwa.
Aimeipongeza pia Sekretarieti ya maadili kwa Viongozi wa Umma chini ya Kamishna Jaji mstaafu Nsekela kwa kuendesha mafunzo haya ili kujenga uelewa kwa viongozi hasa katika Mkoa wa Shinyanga tangu mwezi Juni, 2019 kwa njia mbalimbali.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Gulamhafidh Mukadam aliyeshiriki pia mafunzo hayo amesema mafunzo yanawakumbusha na kuwakosoa pale walipokwenda kinyume na kumshukuru Rais Magufuli kwa utendaji wake ambapo amesema kuwa ni kweli nchi imebadilika sana.
Mmoja wa washiriki Bw. Nila Mabula ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa ndani katika Sekretarieti ya Mkoa, akitoa neno la shukrani baada ya mafunzo, amesema kuwa wanaishukuru sana Sekretarieti kwa mafunzo hayo na kuwasihi washiriki kuyazingatia na kuyashusha kwa watumishi wa chini ili kufikia lengo. Akiongeza kuwa, faida yake ni kuongeza ufanisi katika kazi kwenye nyanja zote.
"Kanuni tulizotajiwa zimetajwa pia hata kwenye vitabu vya dini, hivyo kuzingatia ni kufuata pia maneno ya Mungu" amesema Bw. Nila.
Viongozi na watendaji mbalimbali ngazi ya Mkoa wameshiriki mafunzo hayo ya siku moja wakiwemo Wakuu wa vyombo vya Usalama, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Makatibu Tawala wa Wilaya, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Idara na Vitengo, watendaji wa Mahakama na Wakuu wa Taasisi za Umma.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa