Na. Paul Kasembo, SHY RS.
AFISA Biashara kutoka Ofisi ya Mkuu Mkoa wa Shinyanga Bi. Rose Tungu amewataka wafanyabiashara dogondogo Manispaa ya Shinyanga kujitokeza kusajiliwa na kutambuliwa ili waweze kupata kadi za utambuzi kwani Serikali kupitia Halmashauri ina malengo ya kuwasaidia kwa kuwapatia mikopo maaulumu ya asilimia 7 na waweze kukuza na kuboresha biashara zao.
Ameyasema haya leo tarehe 8 Januari, 2025 wakati akitoa elimu kwa wafanyabiashara Kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga kuhusu umuhimu wa kusajiliwa kwenye mfumo ambapo pamoja na yote amesema zoezi hili litakuwa ni endelevu na tayari limeshaanza katika maeneo yote.
“Ninawahimiza wafanyabiashara wote kujitokeza kwa wingi kusajiliwa ili muweze kutambulika na kupata kadi za biashara ambapo kupitia kadi hizi mtapata fursa mbalimbali ikiwemo kupewa mikopo maalumu ya asilimia 7 ambayo itawasaidia kuboresha na kukuza biashara zenu,” amesema Bi. Rose.
Akizungumzia kuhusu sifa za kupata mikopo ya asilimia 7 Afisa Maendeleo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Bestina Gunje amewasihi wafanyabiashara kutumia fursa hii kujitokeza kwa wingi kujisajili kwani zoezi hili ni endelevu na linalenga kuwasaidia wafanyabiashara kunufaika na mikopo hii ambayo Serikali itatoa ili kuwasaidia kuinua biashara zao hivyo kuwaepusha na mikopo yenye riba kubwa (kausha damu).
Kwa upande wake Afisa Uhusiano Benki ya NMB - Manonga ndugu Filbert Busiri amesema Serikali imetoa Shilingi Bilioni 18 kwa Benki ya NMB kwa Mkoa wa Shinyanga unatarajiwa kupokea takribani Shilingi Milioni 140 ambazo zitatolea kama mikopo Wafanyabiashara ambao tayari wamesajiliwa katika mfumo wa kidigitali na wanaofanya katika maeneo yanayotambulika.
Zoezi la Usajili wa wafanyabiashara ndogondogo lilianza tarehe 19 Februari, 2024 ambapo Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu ndio inaratibu zoezi hili.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa