KATIBU Tawala Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha, amewaomba Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kutumia taaluma zao kuisaidia hospitali kukamilisha miradi ya ujenzi kwa haraka ili kuleta tija na kuwasaidia wananchi kupata huduma bora.
CP. Hamduni ameyasema haya leo Februari 11, 2025 wakati akizindua Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga, kikao kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Vigimark ambapo pamoja na yote amewapongeza wajumbe wote kwa kuteuliwa na Waziri mwenye dhamana ya Afya na kuwataka kutimiza majukumu yao kwa bidii.
“Ninawapongeza wajumbe wote kwa kuteuliwa kwenu na ninawaomba sasa mkatumie vema taaluma zenu ili kuisaidia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga na kukamilisha miradi ya Ujenzi kwa haraka ili kuleta tija na kuwasaidia wananchi kupata huduma bora zaidi, lakini pia itasaidia kuongeza makusanyo ya fedha bila kuathiri huduma kwa wananchi” amesema RAS CP. Hamduni
Akizungumza kwenye uzinduzi wa bodi hiyo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga Daktari Luzila John amesema Hospitali hii inatarajia kuwa na jumla ya majengo 25 ili kukidhi utolewaji wa huduma mbalimbali zenye hadhi ya Hospitali ya Rufaa.
Aidha Makamu Mwenyekiti wa Bodi Daktari John Majigwa pamoja na mambo mengine ametoa shukrani kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi hiyo Ndg. John Majiko ameahidi kuwa watafanya kazi kwa uwezo na weledi wao wote, nguvu zao zote na kwa bidii ili kukamilisha miradi ya ujenzi na kuinua huduma za afya za hospitali.
Uwepo wa Bodi ya Ushauri katika Hospitali ya Mkoa unatajwa kwenda kuongeza tija, kuboresha na kuongeza usimamizi wa karibu katika utoaji wa huduma kwa wananchi na kwa watumishi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga jambo ambalo litapekea kuongezeka pia kwa mapato ya kwa Hospitali na Serikali kwa ujumla.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa