Na. Paul Kasembo, SHY RS.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamiringi Macha amewataka wakandarasi wa barabara waliopata zabuni kuwa wazalendo na waadilifu wanapokwenda kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara katika Mkoa wa Shinyanga huku akiwasisitiza kufanya kazi kwa bidii, weledi, uzalendo na kuzingatia viwango bora vya barabara.
RC Macha Ameyasema haya leo tarehe 4 Oktoba, 2024 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakati akishuhudia hafla ya utiaji saini mikataba 33 ya matengenezo ya barabara za TARURA mkoani Shinyanga kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Hafla hii ambayo pia imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni, Mkuu wa DC wa Kahama Mhe. Mboni Mhita na wadau wengine inajumlisha wakandarasi 21 katika miradi ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa Km. 716, mitaro yenye urefu wa Mita 5,280 madaraja madogo 381, makubwa 4, uwekaji wa taa za barabarani pamoja na barabara ya lami yenye urefu wa Km. 2.8 huku thamani ya miradi ni zaidi ya bilioni 10.
“Ninawataka wakandarasi wote 21 ambao mmepata zabuni hii ya ujenzi wa barabara kuwa na uzalendo, uadilifu, weledi na ubora wa kazi mnapokwenda kutekeleza miradi hii kwa sababu Serikali kupitia fedha za ndani imetoa pesa nyingi ili kuhakikisha inakamilika na kuwanufaisha wananchi wetu ambao ndiyo walengwa," amesema RC Macha.
Akiwasilisha taarifa ya miradi ya ujenzi, Meneja wa Wakala wa Barabara wa Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Shinyanga Mha. Avith Theodory amesema wamepokea fedha za miradi hii kutoka kwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia vyanzo vya mfuko wa barabara, tozo ya mafuta na mfuko wa jimbo huku akisema anayo imani kuwa wakandarasi waliopata zabuni hii wataenda kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mikataba ili kufikia malengo kusudiwa.
Miradi hii ya ujenzi inatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2025 huku ikitegemewa kuwanufaisha wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kwa kutoa ajira zenye zenye ujuzi mdogo kwa jamii inayozunguuka maeneo ya miradi.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa