Na. Paul Kasembo, KISHAPU DC.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewakumbusha wakulima wa zao la pamba kuacha tabia ya kuchanganya na mazao mengine kwenye shamba moja huku akisisitiza pia juu ya umuhimu mkubwa wa kung'olea maotea kwani tupo nyuma ya wakati.
RC Macha ameyasema haya leo tarehe 9 Novemba, 2024 katika mkutano wa hadhara uliolenga kuwakumbusha wakulima wa pamba katika Kitongoji cha Mwabusiga wilayani Kishapu wakulima ambao pia wamepata elimu na ushauri wa namna bora ya kulima eneo dogo kwa tija zaidi na Balozi wa Pamba nchini ndugu Aggrey Mwanri.
"Ndugu zangu wakulima wa zao la pamba hapa Mwabusiga, niwaombe sana na kuwakumbusha kwa dhati kabisa kuacha tabia ya kuchanganya zao la pamba na mazao mengine katika shamba moja, kwa kufanya hivyo hatutaona mafanikio tarajiwa kutoka kwenye kilimo hiki na hakutakuwa na maana yoyote tena ya kulima pamba," amesema RC Macha.
Awali akitoa hamasa ya kilimo cha pamba Mwanri amesema kuwa tumekuwa tukifanya makosa makubwa sana kuchelewa kung'olea maotea na kuondoa masalia katika zao la pamba kwakuwa madhara yake ni makubwa sana ambapo amesema kwa mujibu wa utaratibu wa kilimo bora masalia na maotea hupaswa kuondolewa kabla ya tarehe 15 Septemba, 2024 na ukichelewa kufanya hivyo unazalisha pamba mapepe na isiyokuwa na ubora unaotakiwa.
"Niwaombe sana ndugu zangu Wanabusiga tuendelea kufuata ushauri na maelekezo ya wataalam wetu wa kilimo na wengine ili tuweze kuwa na kilimo bora cha kisasa ambapo utapaswa kulima eneo dogo na lenye kukuletea tija zaidi na tusichanganye mazao katika shamba moja na tung'olee maotea na kuondoa masalia kabla ya kuanza kilimo cha msimu unaofuata," amesema Mwanri.
Aidha ndg. Buluma Kalidushi ambaye ni Mkaguzi wa Pamba Kanda ya Magharibi amewataka wakulima kuzingatia Sheria ya Pamba Na. 2 ya mwaka 2001 na marekebisho yake ya mwaka 2009 iliyotengenezewa Kanuni za mwaka 2011 na hasa kanuni ya 14 kanuni ndogo (1) inaweka katazo la kustawisha na kuuza pamba itokanayo na masalia ya miti ya pamba.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa