KATIBU Tawala Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni amewaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga na Kahama kuhakikisha wanatenga Chumba/Vyumba maalum kwa ajili ya kutumia kama ofisi za Dawati la Huduma za Ustawi wa Jamii na ambavyo vitakuwa vikipatikana katika Stendi zao za Mabasi huku akiwataka kwenda kuhakikisha wanapunguza kabisa kama siyo kuokoa kabisa watoto wanaokimbilia katika Majiji makubwa.
Hayo yanesemwa leo tarehe 11 Februari, 2025 wakati akifungua Kikao cha Utambulisho wa Uanzishwaji wa Dawati la Huduma za Ustawi wa Jamii kwa Stendi Kuu ya Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga (Manyoni) na Kahama kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na kuhudhuriwa na wajumbe mbalimbali kutoka TAMISEMI, Shirika la Railway Children Africa (RCA), Ofisi ya RPC Mkoa wa Shinyanga, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Sekretarieti ya Mkoa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
CP. Hamduni ameipongeza sana Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwa kushirikiana na Shirika la Railway Children Africa (RCA) kwa kuleta mradi huu katika Mkoa wa Shinyanga pamoja na Mikoa mingine na kwamba anaamini kupitia mafanikio yaliyoonekana katika Mikoa ya Mwanza na Dar Es salaam ndio imepelekea mradi kupanuka katika Mikoa mingine 10 ikiwemo Shinyanga zaidi ili kunusuru hali ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani.
Mkoa wa Shinyanga ni moja ya Mikoa yenye changamoto ya watoto wanaoshi na kufanya kazi mtaani hususani katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama ambapo wanapokea mpaka watoto wanaotoka Nchi za jirani.
Changamoto hii imepelekea watoto hao kujifunza na kujiingiza katika tabia hatarishi zaidi na wakati mwingine kutumwa na watu wazima katika matukio ya wizi, uporaji, biashara ya ngono, ulevi na matumizi ya dawa za kulevya na jitihada ambazo zimekuwa zikifanyika kupitia Halmashauri, Idara ya Uhamiaji na Polisi ni kuwabaini kuwafanyia tathmini, kuwahifadhi sehemu salama na kisha kuwaunganisha na familia zao.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa