Na. Paul Kasembo, SHY RS,
MWAKILISHI wa Katibu Tawala Msaidizi Afya, Lishe na Ustawi Mkoa wa Shinyanga Mjiolojia Faustine Mulyutu amewataka wanahabari kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kuwa wanaijenga, kuisitawisha na kuitunza jamii isiyokuwa na maambukizi ya ugonjwa wa Malaria kwani Tanzania bila Malaria inawezekana.
Mulyutu ameyasema haya leo tarehe 6 Januari, 2025 katika Kikao Kazi cha Uhamasishaji Kampeni ya Ugawaji wa Vyandarua kwenye Kaya bila malipo, ambapo kampeni hii inatarajiwa kutekelezwa katika Halmashauri zote 6 za Mkoa wa Shinyanga huku ikitajwa kuwa zaidi ya vyandarua takribani Milioni 1.5 vyenye dawa vitawafikia wananchi lengwa.
“Ninawasihi mkatumie Kikao Kazi hiki kwenda kuijenga, kuisitawisha na kuitunza jamii isiyokuwa na maambukizi ya ugonjwa wa malaria kwani Serikali inaendelea kupiga vita ugonjwa huu ambao unarudisha nyuma kasi ya maendeleo ya nchi yetu, hivyo kupitia jukwaa hili naamini mtaenda kuwahamasisha wananchi ili kwa pamoja tuijenge Tanzania isiyokuwa na Malaria,” amesema Mulyutu.
Kwa upande wake Mdhibiti wa Wadudu Dhurifu Ofisi ya Rais - TAMISEMI Best Yoram amesema kupitia kampeni hii itaenda kuwasaidia wajumbe kuunga mkono jitihada za Serikali za kupinga malaria kwa kuielimisha jamii ili kuhakikisha kwamba asilimia 80 ya kila kaya inamiliki chandarua ili kujikinga na ugonjwa huu.
Naye Afisa Mradi - Malaria kutoka Wizara ya Afya amewasihi wajumbe kutumia jukwaa hili kuihabarisha jamii juu ya matumizi sahihi ya vyandarua kwani baadhi ya wanajamii wamekuwa na dhana potofu juu ya matumizi ya vyandarua hivyo watumie fursa hii kuisaidia jamii kuhusu umuhimu wa kutumia vuandarua vyenye dawa.
Akiwasilisha taarifa ya zoezi zima la ugawaji wa vyandarua, Afisa Mpango wa Taifa wa Udhibiti Malaria kutoka Wizara ya Afya Peter Gitanya amesema kampeni hii itasaidia kuleta vyandarua sawa sawa na idadi ya watu kwani mpaka sasa zoezi la usajili wa kaya limeshaanza na kufikia tarehe 16 Januari, 2025 vyandarua vinategemewa kuanza kusambazwa kwa wananchi ambao wameshasajiliwa.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa