Na. Paul Kasembo, SHY RS.
MWAKILISHI wa Mganga Mkuu Mkoa wa Shinyanga Daktari. Faustine Mulyutu amewaasa wanahabari ambao wamehudhuria mafunzo haya ya m-mama kutumia vizuri yale waliyojifunza kuijulisha jamii juu ya utoaji na utumiaji wa namba 115 ili kuhakikisha inaenda kutengeneza afya ya mama na mtoto pindi dharula inapotokea.
Ameyasema haya tarehe 5 Novemba, 2024 wakati akizungumza na wanahabari kutoka Redio za Kijamii mbalimbali zilizopo ndani ya Mkoa wa Shinyanga, Tabora, Simiyu na Kigoma kwenye mafunzo ya huduma ya usafirishaji wa dharula kwa wajawazito waliojifungua ndani ya siku 42 na watoto wachanga ndani ya siku 28 (m-mama) ambayo yamefanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Vigimark iliyopo Manispaa ya Shinyanga.
“Wanahabari na vyombo vyenu vya kutolea habari mnayo nafasi kubwa sana ya kuisaidia jamii kuelewa vizuri na kwa undani kuhusu huduma ya m-mama ambayo inalenga kuwasaidia akina mama wajawazito na watoto wao wachanga pindi wanapopata dharula na kuhitaji matibabu, hivyo mtumie mafunzo haya kwenda kuwasaidia kufikisha elimu ya matumizi sahihi ya kupiga 115 ambayo ni bure ili wapate msaada wanapouhitaji” amesema Mlyutu.
Aidha amemuomba mratibu wa mafunzo ya m-mama Mkoa wa Shinyanga kuandaa ratiba ya waratibu wa huduma ya afya ili watimize jukumu la utoaji wa elimu ya afya kupitia redio za jamii ili kufikisha ujumbe kwa wanajamii kuhusu huduma hii ya dharula kwa mikoa yote 4 iliyoshiriki mafunzo huku Shinyanga ikitajwa kuwa ya kwanza kutembelewa.
Akiwasilisha mafunzo kwa wanahabari, Mratibu wa mfumo wa m-mama ambaye pia ni Muuguzi Mkuu Mkoa wa Shinyanga Bi. Flora Kajumulla amesema mfumo wa m-mama umetengenezwa kuwa endelevu na nafuu zaidi kwani Serikali imeanzishwa dawati la msaada mtandaoni kwa kila Mkoa nchini ili kuripoti matatizo yoyote ya m-mama huku madereva 4000 tayari wamesajiriwa kutoa huduma ya usafiri.
Huduma ya m-mama inapatikana bure sehemu popote Tanzania kwa kupiga namba 115 ili kuwasiliana na waratibu wa mfumo wa m-mama ambapo mpaka sasa zaidi ya rufaa za akina mama 80,000 na watoto wachanga 17,750 zimesafirishwa.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa