Na. Paul Kasembo, SHY RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewaku,busha wananchi wa Shinyanga kuendelea kuuenzi na kuulinda Muungano wetu kwa kudumisha amani, upendo na mshikamano huku akiwataka kupanda miti na kuitunza ili kuimarisha mazingira yetu ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Ameyasema hayo Aprili 26, 2025 wakati wa kuadhimisha miaka 61 ya Muungano katika Mtaa wa Kalogo, Manispaa ya Shinyanga ambapo kulifanyika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na kufanya usafi wa mazingira, kupanda miti na matembezi ambayo yalianzia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa maadhimisho ambayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Dini, Taasisi, watumishi na wananchi wakiongozwa na Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni.
"Tunapoadhimisha miaka 61 ya Muungano wetu napenda niwakumbushe Wanashinyanga kuendelea kuuenzi na kuulinda kwa kudumisha amani, upendo na mshikamano huku akiwataka kupanda miti na kuitunza ili kuimarisha mazingira yetu ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianch ," alisema RC Macha.
Kando na ukumbusho huo, RC Macha ametumia nafasi hiyo pia kumpongeza na kumshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Hussein Ali Mwinyi kwa kuendeleza Muungano, kuuenzi na kuufanya uendelee kudumu na kuwa bora zaidi.
Huku akiwakumbusha wananchi kujiandaa na zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Mpiga Kura mwezi Mei, 2025 na Uchaguzi Mkuu wa Waheshimiwa Madiwani, Wabunge na Rais ambao huchaguliwa kwa mujibu wa Katiba ya Nchi yetu kila baada ya miaka mitano.
Maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano yanaongozwa na kaulimbiu ”Muungano wetu ni Dhamana, Heshima na Tunu ya Taifa: Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025”.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa