Na. Paul Kasembo, SHY RS.
AFISA Elimu Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi ndg. Dedan Rutazika aliyemuwakilisha Dafroza Ndalichako ambaye nji Katibu Tawala Msaidizi, Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mkoa wa Shinyanga amefungua rasmi mafunzo ya awali ya ualimu na uamuzi wa mpira wa mikono kwa walimu kutoka shule mbalimbali za msingi na sekondari mkoani Shinyanga huku akiwasisitiza kwenda kuyatumia vema mafunzo watakayoyapata hapa ili yawe na tija katika shule wanazotoka.
Rutazika ameyasema haya leo tarehe 1 Agosti, 2024 katika shule ya sekondari Uhuru ambapo mafunzo haya yanafanyika na kuhudhuriwa pia na baadhi ya walimu kutoka Mkoa wa Simiyu na shule binafsi ikiwemo Kom Sekondari mafunzo ambayo yanaongozwa na Mkufunzi wa mchezo huu kutoka Chama cha Mpira wa Mkojo Taifa (TAHA) ndg. Emmanuel Majura.
"Niwasisitize sana walimu wetu ambao mnapata taaluma hii hapa na kupitia mafunzo haya muende kuyatendea haki kwa kuhakikisha yanaleta tija zaidi katika maeneo mnayotoka ili lengo la mafunzo haya likaonekane kwa vitendo na kwa kufanya vizuri katika mashindano yajayo mwaka 2025 kwakuwa ninaimani elimu hii itakuwa imewafikia kwa sehemu kubwa sana wanafunzi wetu hivyo watafanya vizuri zaidi," amesema Rutazika.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Mkono Mkoa wa Shinyanga ndg. Mtaki Musiba amesema kuwa maoni, ushauri na maelekezo wamepokea na watakwenda kuyafanyia kazi ili lengo la kuinua na kukuza wanamichezo wa mpira wa mkono Mkoa wa Shinyanga linafanikiwa.
Aidha Bi. Jesca Simuchile ambaye ni Afisa michezo Mkoa wa Shinyanga amesema kuwa uwepo wa mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Prof. Siza Tumbo aliyeelekeza kuanzishwa kwa program maalum ya kuibua, kukuza na kuimarisha michezo mashuleni ikiwemo na mchezo wa mpira wa mkono mkoani Shinyanga kwani michezo ni afya, ajira na huleta amani.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa