Kata ya Songwa, Wilayani Kishapu imepanga kutumia jumla ya sh. 291,097,581 kati ya sh. milioni mia nne (400,000,000) zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika kituo cha Afya.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Nyabaganga Taraba ametoa taarifa hiyo leo wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack yenye lengo la kukagua miradi ya Afya na Maji Wilayani hapo.
Mhe. Taraba amesema, kati ya shilingi milioni 400 iliyotolewa na Serikali mwezi Januari mwaka huu, kituo hicho kitatumia shilingi 291 katika ujenzi wa miundombinu hiyo ambayo ni nyumba ya mtumishi, maabara, jengo la mama na mtoto, jengo la upasuaji na chumba cha kuhifadhia maiti.
Amesema fedha itakayobaki ambayo ni sh. milioni 108,902,419 imepangwa kutumika kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ya maji, kichomea taka pamoja na shimo la kutupa kondo la nyuma.
Mhe. Mkuu wa Mkoa ameweza kujionea hali ya ujenzi wa miundombinu hiyo ambao upo katika hatua ya awali, hadi sasa kiasi cha sh. milioni 39, kimeshatumika.
Kituo hicho cha Songwa ni moja ya vituo vilivyo katika mpango wa Serikali wa kukarabati vituo vya Afya ili viweze kutoa huduma za dharura za upasuaji, ambapo wananchi zaidi ya 6000 watanufaika na ujenzi huo.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa