Waziri wa maji Mhe. Profesa Makame Mbarawa amewahakikisha wananchi wa vijiji vya Mwakitolyo, Wilaya ya Shinyanga na Kishapu Wilayani Kishapu kuwa tatizo la kukosa maji litakuwa historia baada ya kupewa ahadi hiyo kwa muda mrefu bila ya mafanikio.
Akizungumza na wananchi wa vijiji hivyo kwa nyakati tofauti wakati wa ziara yake Mkoani hapa jana tarehe 04/07/2019, amewaeleza wananchi wa kijiji cha Kishapu kuwa, Serikali inatambua shida ya maji ya muda mrefu inayowakabili hivyo Mamlaka ya Maji Kahama na Shinyanga (KASHWASA) itaanza kujenga mradi katika Wilaya ya Kishapu kwani ina uwezo mkubwa wa kujenga miradi ya maji bila kutumia wakandarasi ambao wanatumia muda mrefu.
"Serikali pesa tunayo na nitaitoa pesa hiyo hivi karibuni, hivi sasa hatutaki msubiri tena kwa muda mrefu, tuliahidi na lazima tutekeleze Ilani" amesama Prof. Mbarawa. Amesema haiwezekani wananchi wa Kishapu wapate shida wakati bomba lipo kilometa chache kutoka hapo.
Aidha, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo Mhe. Mbarawa amesema anajipa miezi mitatu pamoja na KASHWASA kuhakikisha mradi wa maji kutoka kwenye bomba kubwa la maji ya ziwa Viktoria uliopo kilometa 13 kutoka kijijini hapo unakamilika. "Nimetembea maeneo mengi lakini hapa kweli mna shida ya maji, ndoo moja sh. 500 hii haikubaliki, mradi wa awali haukuwa na uwezo kwa sababu mkandarasi na mshauri walifanya ujanja na wizi wa kupindukia"
Amesema yeye akiwa mwenye dhamana ya kuhakikisha wananchi wanapata maji hivyo Serikali imeamua kubadilisha miundombinu yote ya mradi wa awali ambao umeshindwa kufanya kazi na kuanza upya ujenzi wake na kuweka bomba jipya na pesa tayari ipo.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa