Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amewaonya waendesha pikipiki, maarufu kama Bodaboda wenye tabia ya kuwapakia wanafunzi hasa wa kike na kuwalaghai matokeo yake kuwapa mimba za utotoni.
Mhe. Telack ametoa onyo hilo mapema leo tarehe 31 Januari, 2019, wakati akitoa hotuba ya kufunga mradi wa “DREAMS – Innovation Challenge, keeping girls in Secondary schools” uliokuwa unatekelezwa na shirika la “amref health Africa” kwa miaka miwili katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, Wilaya ya Kahama.
“Suala la bodaboda tumeshalisema sana, itabidi kukaa vikao na viongozi wa bodaboda, vijiwe vya boda boda vilivyopo karibu na shule viondolewe, watafute wateja siyo wanafunzi” amesema Telack.
Akisisitiza jambo hilo Mhe. Telack amewataka Wakuu wa Wilaya kuhakikisha bodaboda wenye tabia ya kuwapatia “lift” wanafunzi wa kike waache mara moja na wakibainika wakamatwe.
Aidha, amewahimiza wanafunzi watembee kwenda shule badala ya mazoea ya kupanda bodaboda ili kuwaepusha na vishawishi visivyo vya lazima.
Amesema, mtoto wa kike ni rasilimali, hivyo wakiachwa bila uangalizi ni kuharibu Taifa la baadaye matokeo yake hata familia zao hazitadumu kutokana na kuanza ngono mapema.
Katika hotuba yake, Mkuu wa Mkoa pia ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kuendeleza mazuri yaliyofanywa na mradi wa DREAMS ili kuwasaidia wanafunzi hasa wa kike, kwani uelewa wa afya ya uzazi umewasaidia sana kupunguza maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI kwa vijana kutoka asilimia 2.5 mwaka 2016 hadi 0.8 mwaka 2018.
Mradi wa DREAMS uliowafikia wanafunzi katika shule 15 ndani ya Halmashauri ya wilaya ya Msalala, umepunguza tatizo la watoto wa kike walioacha shule kwa sababu ya mimba kutoka wanafunzi 79 mwaka 2016 hadi wanafunzi 38 mwaka 2018.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa