#shinyanga_rs
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha, ameahidi kuendeleza juhudi za Serikali katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimekuwa na madhara kwa mazingira na maisha ya wananchi wa mkoa huo.
Kauli hiyo imetolewa leo Juni 17, 2025 wakati alipokutana na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis alipotembelea ofisi kwake ambapo ujio wa Mhe. Khamis umekuja sambamba na Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame yatakayofanyika mkoani Shinyanga.
Akizungumza ofisini kwake, RC. Macha alieleza kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo ukame na kupungua kwa uoto wa asili, zimeathiri kwa kiasi kikubwa ustawi wa jamii na kwamba Mkoa wa Shinyanga umejipanga kuongeza kasi ya utekelezaji wa kampeni ya upandaji miti, utoaji wa elimu kwa jamii juu ya uhifadhi wa mazingira, na kushirikiana na wadau katika utekelezaji wa miradi ya kijamii.
"Shinyanga ni miongoni mwa Mikoa inayokabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi. Tumejipanga kuhakikisha tunashughulikia changamoto hizi kwa kushirikiana na sekta binafsi, wananchi na taasisi mbalimbali," alisema Mhe. Macha.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mhe. Khamis alisisitiza umuhimu wa utekelezaji wa mikakati ya Kitaifa ya mazingira kwa vitendo katika kila Mkoa. Alibainisha kuwa mafanikio ya mapambano dhidi ya jangwa na ukame yanategemea mshikamano na ushirikiano wa wadau wote kwa pamoja.
Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika Kitaifa mkoani Shinyanga, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itatekeleza shughuli kadhaa ikiwemo upandaji miti, utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu uhifadhi wa mazingira, pamoja na kufanyika kwa mkutano wa kitaalamu uliowahusisha wadau mbalimbali katika ukumbi wa Karena Hotel, Manispaa ya Shinyanga.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa