Na Johnson James Shinyanga
Maafisa Utamaduni kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Shinyanga wamekutana leo katika ukumbi mdogo wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwenye kikao kazi maalum kilichofanyika kwa lengo la kujadili namna bora ya kusimamia maktaba za video, pamoja na kubadilishana uzoefu kuhusu ukusanyaji wa mapato kupitia maktaba hizo, pamoja na vyanzo vingine vya mapato.
Kikao hicho kimefanyika chini ya uratibu wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Kitengo cha Utamaduni, ambapo ajenda kuu zilijikita katika kutoa elimu ya utafiti kwa wamiliki wa maktaba za video na kujadili changamoto na mafanikio katika ukusanyaji wa mapato kwenye halmashauri mbalimbali.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Afisa Utamaduni wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Janeth Elias Mompome amesema sekta ya Sanaa kupitia maktaba za video ni miongoni mwa maeneo yenye mchango mkubwa kwenye mapato ya halmashauri, lakini bado yanakabiliwa na changamoto za usimamizi, ufuatiliaji na usajili rasmi wa wamiliki.
"Ni muhimu sasa kuimarisha usimamizi wa maktaba hizi kwa kushirikiana na wamiliki wake. Kupitia utafiti na elimu kwao, tutaweza kuongeza mapato halali ya serikali na kukuza sekta ya utamaduni kwa ujumla," alisema.
Washiriki wa kikao hicho walipata nafasi ya kuwasilisha uzoefu wa kila halmashauri juu ya namna wanavyokusanya mapato kutoka kwa wamiliki wa maktaba hizo, changamoto wanazokutana nazo, pamoja na mapendekezo ya maboresho ya mifumo ya usimamizi.
Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa ni pamoja na kuanzisha utaratibu wa kutambua rasmi maktaba zote zinazofanya kazi katika mkoa, kuwaelimisha wamiliki kuhusu umuhimu wa kulipa ushuru halali, na kutumia mfumo wa kidigitali katika kufuatilia shughuli zao kwa uwazi zaidi.
Kikao hicho pia kimeweka msingi wa kuandaa mkakati wa pamoja wa mkoa wa kusimamia sekta ya video libraries kwa ufanisi zaidi, huku msisitizo ukiwekwa kwenye ushirikiano baina ya halmashauri, wamiliki na mamlaka nyingine zinazohusika na masuala ya sanaa na utamaduni.
MWISHO
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa