Na Johnson James – SHINYANGA
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita @mboni_mhita leo Novemba 11, 2025 amekutana na kufanya mazungumzo na Msanii wa muziki wa kizazi kipya kutoka Shinyanga, Bando MC aliyeongozwa na Afisa Utamaduni Mkoa, Janeth Mompome alipomtembelea ofisini kwake kwa lengo la kuonesha mshikamano na kuthamini mchango wa Serikali katika kuinua sekta ya sanaa nchini.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mhita amempongeza Bando MC kwa kuwa mfano bora kwa vijana kwa kutumia kipaji chake si tu kwa burudani, bali pia kama nyenzo ya kuelimisha na kuhamasisha maendeleo katika jamii.
Mhe. Mhita ameongeza kuwa Serikali ya Mkoa wa Shinyanga itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wasanii na vijana kwa ujumla, kwa kutambua kuwa sanaa ni moja ya maeneo yenye fursa kubwa za ajira, ubunifu na maendeleo ya kiuchumi.

“Ni jambo la kuigwa kuona msanii anatumia kipawa chake kusaidia wengine. Tunathamini jitihada hizi na tunawahamasisha vijana wengine kuiga mfano huu,” amesema Mhe. Mhita.
Katika kikao hicho, Mussa Mabumo Maarufu kama Bando MC @bando_tz ameeleza kuwa anatarajia kuandaa tamasha la muziki Novemba 22, 2025, litakalolenga kurudisha shukrani kwa jamii kwa kusaidia vijana 30 wa Shinyanga waliopo kwenye biashara ndogondogo kwa kuwapatia vifaa vya kuwawezesha kiuchumi.
"Nia yangu ni kuonyesha kuwa sanaa inaweza kuwa chombo cha mabadiliko. Kupitia tamasha hili, nataka kusaidia vijana wenzangu kusonga mbele," amesema Bando MC.

OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa