Na Johnson James,Shinyanga
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, ametoa wito kwa wafanyabiashara na wawekezaji kuchangamkia fursa za kiuchumi zilizopo katika Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kukuza uchumi wa mkoa huo na Taifa kwa ujumla.

Mhe. Mhita ametoa wito huo leo Novemba 13, 2025 wakati wa Mkutano ulioambatana na uzinduzi wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Shinyanga, uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, wawakilishi wa sekta binafsi, wafanyabiashara na wadau wa maendeleo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mhita ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Shinyanga, amesema Mkoa huo umejaliwa kuwa na rasilimali nyingi na fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, mifugo, madini, viwanda na biashara, hivyo kuna haja ya kuzitumia fursa hizo kikamilifu kwa maendeleo ya uchumi wa mkoa na Taifa.

“Napenda kuwahamasisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya mkoa kuchangamkia fursa zilizopo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya pamba, bidhaa za mifugo, pamoja na huduma za kijamii kama shule, hospitali na hoteli. Pia, Mkoa umetenga maeneo rasmi ya uwekezaji likiwemo eneo la Buzwagi Special Economic Zone ambalo tayari limepata leseni kutoka TISEZA,” amesema Mhe. Mhita.
Aidha, Mhe. Mhita amesisitiza kuwa Mabaraza ya Biashara ni majukwaa muhimu yanayowakutanisha wadau wa sekta binafsi na Serikali kwa pamoja kujadili namna bora ya kuboresha mazingira ya biashara na kutatua changamoto zinazokabili sekta hiyo ili kuimarisha mchango wake katika kukuza uchumi.
Awali, akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Kamishna wa Polisi Salum Hamduni, alieleza kuwa mabaraza hayo ni daraja muhimu kati ya Serikali na Sekta Binafsi katika kubaini changamoto na fursa mbalimbali kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Shinyanga, Bw. Jonathan Manyama, aliipongeza Serikali kwa jitihada zake katika kuboresha mazingira ya biashara.

OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa