Na Johnson James, Shinyanga
Jumla ya wanafunzi 29,193 wanatarajiwa kufanya Mtihani wa Upimaji wa Kidato cha Pili mkoani Shinyanga, ambao unatarajiwa kuanza rasmi Novemba 10 hadi 19 katika shule mbalimbali za sekondari mkoani humo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Afisa Elimu wa Mkoa wa Shinyanga, Samson Hango, kati ya wanafunzi hao, wavulana ni 12,103 na wasichana ni 17,090, huku watahiniwa 42 wakiwa ni wenye mahitaji maalumu.
Hango amewahimiza wazazi na walezi kuhakikisha wanafunzi wote waliojiandikisha wanafika kwenye vituo vyao vya mtihani kwa wakati ili kutimiza wajibu wao wa msingi wa kitaaluma.
"Ni muhimu wazazi na walezi wakawapa wanafunzi motisha na kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kufanya mtihani huu kwa utulivu, kwani ni hatua muhimu katika maendeleo yao ya elimu," amesema Hango.
Aidha, ametoa onyo kali kwa walimu na watumishi wa elimu watakaobainika kuhusika katika vitendo vya udanganyifu au kukwamisha zoezi hilo kwa namna yoyote ile, akibainisha kuwa mtihani huu ni wa upimaji wa kawaida lakini una umuhimu mkubwa kwa kupanga maendeleo ya kitaaluma ya wanafunzi.
Mtihani huu wa upimaji unafanyika kwa lengo la kuangalia maendeleo ya kitaaluma kwa wanafunzi wa kidato cha pili kabla ya kuendelea na ngazi za juu za sekondari.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa