Afisa Utamaduni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Janeth Elias Mompome, amehitimisha kwa heshima kubwa siku ya nne ya Tamasha la Nne la Utamaduni lililofanyika katika Himaya ya UKUNE, kijiji cha Iboja, Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, akisisitiza umuhimu wa kuenzi na kudumisha mila na desturi nzuri za Kisukuma.
Tamasha hilo ambalo limekuwa jukwaa la kipekee la kuonesha utajiri wa tamaduni za kabila la Wasukuma, limebeba ujumbe mahsusi wa kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alilolitoa mwaka 2022 akiwa jijini Mwanza, akihimiza kila mkoa kuandaa matamasha ya utamaduni ili kurithisha urithi huu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Katika tamasha hilo lililofanyika Agosti 22,2025 Halmashauri ya Ushetu, Bi. Janeth alipata nafasi ya kutembelea mashindano ya vikundi mbalimbali vya sanaa ya utamaduni, ambavyo vilionesha vipaji vya kipekee katika ngoma, mavazi, nyimbo na maigizo ya kitamaduni.
Akimpongeza Chifu Mkuu Hangaya kwa kuendelea kulisimamia tamasha hilo kwa mafanikio, Afisa huyo wa Utamaduni alieleza kuwa utamaduni ni uti wa mgongo wa jamii yoyote na unastahili kulindwa kwa gharama yoyote ile.
Katika kilele cha siku hiyo, washindi wa mashindano ya sanaa walitangazwa na Bi. Janeth alikabidhi zawadi kwa vikundi vitatu bora vilivyoibuka kidedea, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za kuhifadhi urithi wa kitamaduni.
Tamasha hilo limeendelea kuwa alama ya mshikamano, urithi na utambulisho wa jamii ya Kisukuma ndani ya Mkoa wa Shinyanga na Tanzania kwa ujumla.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa