Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga imeanza kuchukua hatua thabiti kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 kwa kuwakutanisha waandishi wa habari na kuwapatia mafunzo maalum ya kupinga vitendo vya rushwa katika kipindi hiki nyeti.
Mafunzo hayo yamefanyika Septemba 25, 2025 katika Ukumbi wa Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, yakilenga kuwawezesha wanahabari kuelewa kwa kina Sheria ya Kuzuia Rushwa, Sheria ya Gharama za Uchaguzi, na namna bora ya kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kutumia kalamu na vipaza sauti vyao.
Akifungua rasmi mafunzo hayo, Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Bi. Mwamba Masanja, amesisitiza kuwa vyombo vya habari ni nguzo muhimu ya uwajibikaji katika jamii, na hivyo vina nafasi ya kipekee katika kuelimisha umma kuhusu madhara ya rushwa, hasa wakati huu wa uchaguzi.
"Ni wajibu wenu kuhakikisha elimu hii haibaki humu ukumbini, bali inafika kwa wananchi kupitia vipindi, makala, na mijadala mnayoandaa. Wananchi wakielimika watatambua kuwa kutumia haki yao ya kupiga kura ni hatua ya kuikataa rushwa na kuchagua viongozi wanaofaa,” amesema Bi. Masanja.
Kwa upande wake, Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma TAKUKURU Shinyanga, Bw. Mohammed Doo, amewataka wanahabari kuendelea kuwa mabalozi wa uadilifu, kwa kuhakikisha taarifa wanazochapisha au kutangaza hazichochei au kufumbia macho vitendo vya rushwa, bali zinakuwa sehemu ya ujenzi wa taifa.
“Vyombo vya habari vinaweza kuhamasisha uwajibikaji, kwa kuwafikia wananchi kwa lugha rahisi kuhusu madhara ya rushwa na umuhimu wa kuchagua viongozi bora kwa maslahi ya maendeleo ya taifa letu,” amesema Doo.
Mafunzo hayo yaliambatana na kaulimbiu isemayo:
“Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako na Langu – Tutimize Wajibu Wetu.”
Wanahabari waliohudhuria wamepongeza hatua hiyo ya TAKUKURU, wakiahidi kuwa mabalozi wa mapambano dhidi ya rushwa, hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa