Serikali Mkoani Shanyanga imesema itahakikisha inajipanga kuweka mazingira mazuri na wezeshi kwa watu wenye ulemavu hususani watu wenye ualbino kushiriki katika uchaguzi Mkuu ujao bila ubaguzi wowote kwani wana haki sawa ya kuchagua na kuchaguliwa.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko ametoa kauli hiyo jana tarehe 19/01/2020 wakati akizindua mradi wa Haki Yetu awamu ya pili kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kuwaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri zote Mkoani hapa kuhakikisha wanaweka bajeti kwa ajili ya kuwahudumia watu wenye ulemavu hasa wenye ualbino ikiwemo kuwawezesha kiuchumi..
Mboneko amesema Serikali inatambua juhudi zinazofanywa na wadau wanaopambana na ukatili kwa watu wenye ulemavu na kushukuru shirika la 'Under the same sun" na washirika wake kwa kuanzisha mradi huo muhimu ambao utasaidia kupunguza au kuondoa kabisa ukatili unaofanywa hasa kwa watu wenye ualbino.
Ameongeza pia kuwa, Serikali itaimarisha uhusiano kwa wadau wote wanaotekeleza mapambano dhidi ya watu wenye ulemavu na kuwaomba wahakikishe wanapita kila kata ili wananchi wapate uelewa na kuongeza nguvu katika kupinga ukatili wa waina zote ikiwemo kuondosha mila kandamizi.
"Serikali ya Mkoa imeendelea kukemea, kutoa elimu, kuhifadhi na kuwalinda watu wenye ulemavu kwa kushirikiana na wadau wote pamoja na viongozi wa Dini, ndiyo sababu kwa kipindi kirefu haijasikika taarifa za mauaji ya watu wenye ualbino, bado ukatili wa kijinsia upo hasa kwa wanawake na watoto kwa sababu za kiuchumi, imani potofu, mila kandamizi na kukosa hofu ya Mungu" amesema Mboneko.
Bi. Wakyo Musong'o ambaye ni Meneja mradi wa Haki Yetu amesema kuwa lengo la mradi huo unaotekelezwa kwa kipindi cha mwezi Oktoba 2019 mpaka Juni 2021 katika Mikoa mitano ya kanda ya Ziwa ni kupambana na ubaguzi na vitendo vya kikatili dhidi ya watu wenye Ualbino kwa kuwafikia walengwa zaidi ya milioni 4 kwa njia mbalimbali wakiwemo watendaji, viongozi, wanafunzi na wanajamii kwa ujumla.
Bi. Wakyo amesema malengo mahususi ya mradi ni pamoja na kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu hali za watu wenye ualbino, kuhamasisha uboreshwaji wa sheria na sera na kuimarisha ushiriki wa viongozi wa Serikali na viongozi wa Dini katika kuhamasisha ulinzi kwa watu wenye ualbini na kupata haki kwa waathirika wa ukatil.
Amesema mradi huo unaotekelezwa na mashirika matatu yaani "Under the same sun, CEFA na GNRC awamu ya kwanza ulifikia watu zaidi ya milioni 60.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Afya, kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa Dkt. Rashid Mfaume, amewashukuru wadau hao kwa juhudi wanazofanya kudhibiti mauaji ya watu wenye ualbino kwani wanaisaidia Serikali kwa kiasi kikubwa na kuwaomba kutoacha kutoa elimu kwenye jamii hata kama matukio ya ukatili yanapungua.
Amewataka Waganga wa asili wafanya kazi zao kwa taratibu na miongozo iliyopo na kuwa atakayekiuka na kugundulika anatumia ramli chonganishi hatabaki salama kwani matukio mengi ya mauaji ya watu wenye ualbino chanzo ni Waganga hao.
Naye Mkurugenzi wa shirika la "Under the same sun" Bi. Berthasia Ladislaus amesema anaishukuru Serikali ya Mkoa wa Shinyanga kwa juhudi kubwa za kukomeaha mauaji ya watu wenye ualbino kwa kushirikiana na Viongozi wa dini na wadau mbalimbali, hali iliyochangia kupungua kwa vitendo hivyo.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa awamu ya pili ya mradi wa Haki Yetu unaotekelezwa na shirika la "Under the same sun" kwa kushirikiana na mashirika ya GNRC na CEFA hapo jana katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa shirika la "Under the same sun" Bi. Berthasia Ladislaus na wengine ni wafanyakazi wa shirika hilo, kulia ni Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Afya Dkt. Rashid Mfaume na timu kutoka shirika hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko, akitoa neno la uzinduzi wa mradi huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack
Meneja mradi wa Haki Yetu Bi. Wakyo Musong'o akitoa taarifa ya malengo ya mradi kabla ya uzinduzi wa mradi huo
Mkurugenzi wa shirika la Under the same sun Bi. Berthasia Ladislaus akitoa neno la shukrani kwa Mkoa wa Shinyanga mara baada ya uzinduzi wa mradi wa Haki Yetu
Baadhi ya washiriki wa uzinduzi huo wakifuatilia matukio yanayoendelea, chini ni watoto kutoka shule ya msingi Buhangija katika Manispaa ya Shinyanga
(Picha zote na Marco Maduhu - Shinyanga)
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa