Na. Paul Kasembo, H/M YA MSALALA.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewataka Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kuwatumikia wananchi wao vizuri na kwa weledi zaidi ili waweze kuacha alama nzuri yenye tija kwa wananchi wao kama ishara ya kumbukumbu ya uwepo wao madarakani kwa kipindi ambacho walikuwa wakiwatumikia wananchi wao huku akitoa angalizo kwa watumishi wa Halmashauri kuhakikisha kwamba Hati Safi 3 walizozipata kwa mfululizo ziendane na matendo yao na maadili katika kuwahudumia wananchi wa Msalala.
Mhe. RC Macha ameyasema haya leo tarehe 26 Juni, 2024 alipokuwa akitoa salamu za Serikali katika Baraza Maalum la Madiwani lenye kujadili mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo pamoja na mambo mengine pia ameipongeza sana Msalala kwa kupata hati safi kwa miaka mitatu (3) mfululizo jambo ambalo linatia moyo japokuwa kupata hati hizo haina maana kwamba wao ni wasafi zaidi badala yake wakaishi na kuakisi hati safi hizo.
"Niwatake sasa Waheshimiwa Madiwani mfanye kazi kwa weledi zaidi katika kuwatumikia wananchi ili muache alama njema, nzuri zenye tija na maslahi mapama ya wananchi pale ambapo mtakuwa mmeondoka madarakani, nanyi watumishi muishi kwa matendo na kufanya kazi kwa maadili safi kama hati mlizopata kwa miaka yote mitatu," amesema RC Macha.
Aidha, amesisitiza tena kwa Waheshimiwa Madiwani, watumishi na wananchi wote wa Halmashauri ya Msalala kuhakikisha wanatoa ushirikiano mkubwa kwa wakandarasi na watumishi wanaojenga barabara ya Kahama Kakola Km 74 kwa kiwango cha lami na kwamba ulinzi wa mali zao wakandarasi wakati wote ili mradi huu uweze kujengwa na kukamilika kwa viwango, muda na kwa thamani iliyokusudiwa ili ianze kuleta tija kwa wananchi.
Kwa upande wake CPA. Yusuph Mabwe ambaye ni Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Nje Mkoa wa Shinyanga amewakumbusha Msalala kuhakikisha kuwa wanaongeza jitihada katika kukusanya mapato ya Serikali, kuepuka matumizi ya fedha mbichi na badala yake makusanyo yote yanayofanywa yapelekwe Benki kwa wakati kuepuka hoja zisizokuwa za lazima.
HABARI PICHA
Picha ikimuonesha Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Prof. Siza Tumbo wakati wa mkutano maalum
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa