Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amezundua rasmi kampeni ya kupima virusi vya UKIMWI na kuanza kutumia dawa za kufubaza virusi ARV mapema, katika viwanja vya shule ya msingi Tinde, Kata ya Tinde, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Kampeni hii ya Kitaifa inayoitwa “Furaha yangu – Pima, Jitambue, Ishi”, inasimamiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia mpango wa Taifa wa kudhibiti UKIMWI kwa kushirikiana na mradi wa USAID – Tulonge Afya na wadau wengine.
Akizindua kampeni hiyo Mhe. Telack amewataka wanaume kupima afya zao badala ya kuwaachia wake zao wanapokwenda kupima wajiridhishe na majibu yao. Telack amesema kuwa, kila mtu ana mwili wake hivyo hata kupata maambukizi miili inatofautiana, kwa hiyo wasiridhike na majibu ya wanawake, washiriki pia katika kupima.
Akitoa taarifa ya hali ya ushamiri, Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Rashid Mfaume, amesema bado kiwango cha maambukizi ya UKIMWI kipo juu ya kiwango cha Kitaifa kwa asilimia 5.9 japo kiwango kimeshuka kutoka 7.2 mwaka 2015.
Dkt. Rashid amesema kuwa, Mkoa umeendelea kutekeleza afua mbalimbali kwa kushirikiana na wadau kuhimiza upimaji ambapo hadi hivi sasa tayari 364,361 wananchi wameshapima, Huduma za tohara wanaume waliofikiwa hadi sasa ni 54,868, Huduma za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, Huduma na mafunzo kwa walioathirika.
Amesema Lengo la kampeni ni kuwafikia wananchi ambao hawajatambua hali zao ili wajitambue kwani wanaendelea kuongeza maambukizi kwenye jamii.
Kampeni hii itaendelea kwa muda wa miezi sita katika Mkoa wa Shinyanga.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa