Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. William Lukuvi ametembelea Mgodi wa Nyandolwa uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kufuatia ajali ya kutitia kwa mgodi huo, na kueleza kuridhishwa kwake na kasi ya jitihada za uokoaji zinazoendelea kufanywa na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Kabla ya Waziri huyo kuzungumza na vyombo vya habari na wananchi waliokusanyika katika eneo la tukio, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, alitoa taarifa fupi kuhusu hatua mbalimbali ambazo zimechukuliwa tangu kutokea kwa ajali hiyo. Alieleza kuwa kazi ya uokoaji inaendelea bila kuchoka na Serikali imehakikisha wahusika wote wa usalama na msaada wapo kazini muda wote kuhakikisha maisha yanaokolewa.
Katika ziara hiyo, Mhe. Lukuvi alieleza kuwa Serikali inafuatilia kwa karibu hali ya uokoaji na itaendelea kutoa misaada muhimu kwa familia za waathirika. Ametoa pole kwa familia zilizopoteza ndugu na kusema kuwa serikali imejipanga kugharamia mazishi, pamoja na kutoa usafiri kwa miili ya wale watakaopatikana wakiwa wamefariki dunia.
Aidha, Mhe. Lukuvi amesema kuwa ziara yake ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyetoa agizo kuwa Serikali isimamie kwa karibu shughuli zote za uokoaji na kuhakikisha waathirika wanapatiwa msaada wa haraka, wa kutosha na wa kuwafariji.
"Serikali iko pamoja na wananchi katika kipindi hiki kigumu, na tutaendelea kuhakikisha kila juhudi inafanyika kuwaokoa mafundi waliokwama chini ya kifusi, sambamba na kuwapa faraja wahanga na familia zao," amesema Lukuvi.
Amewapongeza pia viongozi wa Mkoa wa Shinyanga wakiongozwa na RC Mhita kwa kusimamia kwa karibu shughuli za uokoaji, na kuhakikisha usalama na utulivu vinatawala katika eneo hilo la tukio.
Mpaka sasa jumla ya mafundi 11 wameopolewa, ambapo kati yao 8 wamepoteza maisha na 3 wakiwa hai, huku mafundi wengine 14 wakiendelea kutafutwa chini ya kifusi kufuatia ajali hiyo iliyotokea wakati wa shughuli za ukarabati wa mgodi huo zikiendelea.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa