Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini zimetakiwa kutumia mfumo maalumu wa kuajiri na kusambaza watumishi wa kada ya Afya kulingana na uzito wa kazi katika vituo vya Afya na Zahanati.
Katibu Tawala Msaidizi Huduma za Afya katika Sekretarieti ya Mkoa wa Shinyanga Dkt. Rashid Mfaume ametoa wito huo, akifungua kikao kazi cha kuwasilisha matokeo ya zoezi la kubaini mahitaji ya watumishi kwa kutumia mfumo wa WISN plus POA kwa Mikoa ya Mara na Manyara yaliyofanyika Mkoani Shinyanga mapema wiki hii.
Mfumo huo wa WISN plus POA hutumika kukokotoa mahitaji ya watumishi kwa kila kada katika kituo cha kutolea huduma za Afya.
Kwa sasa mfumo huu unatumika kwa ajili ya Vituo vya afya na Zahanati tu, kwa kada mbalimbali zilizopo katika ngazi hizo za utoaji huduma ambazo ni waganga, matabibu, maafisa wauguzi na wauguzi.
Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mradi wa uimarishaji mifumo ya Sekta ya Umma nchini (PS3), pamoja na Taasisi ya Touch foundation walifanikiwa kutengeneza toleo jipya lililorahisishwa la mfumo huo wa WISN plus POA unaouzingatia uzito wa kazi katika vituo vya kutolea huduma ambapo hivyo kupunguza changamoto ya gharama za kutembelea vituo kwa ajili ya kukusanya taarifa kama ilivyofanyika hapo awali.
Kwa upande wake mwakilishi kutoka OR- TAMISEMI, Bw. Elias Magere amesema Halmashauri zote 185 nchini zimeshapata mafunzo ya kutumia mfumo huu ambapo Maafisa Utumishi, Waganga Wakuu wa Mikoa, Makatibu wa Afya na Waratibu wa MTUHA kwa ngazi za Mikoa na Halmashauri walishiriki.
Afisa TEHAMA wa OR – TAMISEMI Bw. Baraka Emmanuel amesema kuwa, mfumo huu unalenga kuimarisha rasilimali watu katika Sekta ya Afya na pia Maafisa Utumishi wataweza kujua mahitaji halisi ya watumishi na kutoa taarifa za watumishi wapya watakaoripoti kwenye vituo vya Afya kwa urahisi.
Bw. Baraka ameongeza kuwa, mfumo utarahisisha mchakato wa ajira za Afya na Serikali kupeleka watumishi wengine haraka zaidi kwenye vituo iwapo watumishi waliopangiwa hawataripoti kwa wakati.
Naye Afisa Rasilimali watu kutoka Mradi wa PS3 Bi. Scholastica Komba amesema kuwa mfumo wa WISN plus POA ni muhimu sana kwa kada ya Afya kwani wananchi watapata huduma za Afya inavyostahili kutokana na uwepo wa watumishi wa kutosha kulingana na mahitaji.
Kikao kazi hicho kilichofanyika kwa makundi kuanzia tarehe 04 hadi 12 Juni, mwaka huu katika ukumbi wa Liga Hotel Mkoani Shinyanga kimejumuisha Mikoa ya Shinyanga, Singida, Simiyu, Mara, Manyara na Mwanza.
Baadhi ya wawezeshaji wa kikao kazi kilichofanyika Mkoani Shinyanga
wakiwa katika picha ya pamoja kutoka kushoto ni Bw. Haruni Mwakilasa
mwakilishi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Bw. Elias Magere wa OR - TAMISEMI,
Bi. Scholastica Komba wa PS3 na Bw. Baraka Emmanuel kutoka OR - TAMISEMI.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa