Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali Watu, David Lyamongi amezitaka Halmashauri za Manispaa ya Shinyanga na Kahama kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya kuendeleza utoaji wa huduma katika madawati ya ustawi wa jamii yaliyopo kwenye stendi za mabasi
Alitoa agizo hilo Septemba 26, 2025 katika kikao cha tathmini ya utoaji wa huduma kwenye madawati hayo yaliyopo stendi za mabasi za Manispaa ya Shinyanga na Kahama, kikao kilichoratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kushirikiana na Shirika la Railway Children Africa (RCA).
Lyamongi amesema lengo la kuimarisha madawati hayo ni kuhakikisha watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani pamoja na makundi mengine yenye uhitaji wanapata huduma za kitaalamu zitakazosaidia kupunguza changamoto wanazokabiliana nazo.
Aidha, amezitaka mamlaka husika kuhakikisha miradi mikubwa ya ujenzi kama vile stendi mpya za kisasa zinazojengwa Manispaa ya Shinyanga na Kahama, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Ibadakuli na vituo vya Treni ya Mwendo Kasi (SGR), inatenga vyumba maalumu kwa ajili ya madawati ya ustawi wa jamii, vyumba vya jeshi la Polisi pamoja na huduma ya kwanza.
Kwa mujibu wake, hatua hiyo itasaidia kupunguza ongezeko la watoto wanaoingia na kuishi mtaani.
Kwa upande wake, Mratibu wa Shirika la RCA, Bi. Irene Wampembe, amepongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Mkoa wa Shinyanga kupitia madawati ya ustawi wa jamii na kusisitiza kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na halmashauri kuhakikisha huduma hizo zinafika kwa walengwa.
Hata hivyo, ameziomba halmashauri kuandaa mikakati thabiti ya uendelevu wa huduma hizo kwani mradi unaotekelezwa na Shirika la RCA unatarajiwa kufikia ukomo wake mwezi Machi 2026.
Kikao hicho kimehudhuriwa na viongozi na wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Halmashauri za Manispaa ya Shinyanga na Kahama, Ofisi ya Latra, Ofisi ya RPC, Uhamiaji, wawakilishi wa wenyeviti wa mitaa, watendaji wa kata, watoa huduma za malezi ya mtoto pamoja na wadau kutoka Shirika la RCA.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa