Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Zainab Chaula amesema Hospitali za Umma zinatakiwa kuwa na mazingira mazuri ya kuwavutia wananchi kukimbilia kupata huduma.
Dkt. Chaula Ameyasema hayo mapema leo tarehe 23/10/2019 wakati wa ziara yake ya kazi Mkoani Shinyanga yenye lengo la kutembelea miradi ya maendeleo na kuzungumza na watumishi.
Dkt. Chaula amesema kuwa, iwapo hospitali za Umma zitakuwa na mazingira ya kuvutia kuanzia upande wa majengo hadi huduma hata watu wasioumwa watapenda kwenda kupata ushauri . "Hospitali zikiimarishwa katika suala zima la huduma na Afya na mambo yote, siyo lazima waje wagonjwa tu, tunataka hata watu wazima wasioumwa waje kupata huduma ya ushauri"
Awali, akimkaribisha Dkt. Chaula, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amemueleza kuwa, kazi kubwa imefanyika katika Serikali ya awamu ya tano hivyo kufanikisha kupunguza changamoto nyingi ikiwemo vifo vya akina mama na watoto kutokana na ongezeko la Vituo vya kutolea huduma za Afya.
" Shukrani kwa Mhe. Rais na watendaji wa Wizara ya Afya, Vituo vipo ni vizuri, wananchi wanavifurahia na vimejengwa kwa gharama nafuu kwa kutumia mafundi wetu" amesema Mhe. Telack.
Katika hatua nyingine Dkt. Chaula ameahidi kuhakikisha fedha iliyobaki kwa ajili ya kukamilisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa inapatikana ili ianze kutoa huduma ikiwemo kununua vifaa tiba na vitendea kazi vingine.
Akizungumza na watumishi, katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga Dkt. Chaula amewakumbusha kutekeleza majukumu yao na kuhakikisha wanawajibika kabla ya kudai haki. Amesisitiza pia wafanye kazi kwa pamoja kama timu moja lengo likiwa wananchi wanapata huduma.
Akiwa Mkoani Shinyanga, Dkt. Chaula ametembelea eneo la Mwawaza inapojengwa Hospitali mpya ya Rufaa ya Mkoa pamoja na kuzungumza na watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa