Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amewataka wananchi kuwatunza wakina mama wajawazito ili kuhakikisha wanajifungua salama katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Mhe. Telack ametoa wito huo wakati akizindua kampeni ya “Jiongeze tuwavushe salama” yenye lengo la kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi leo katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Telack amesema kuwa, vifo vinavyotokana na uzazi bado ni tatizo katika Mkoa wa Shinyanga hivyo kila mmoja katika jamii awajibike ili kuwaepusha akina mama na watoto.
“Tukishikana, tukafanya pamoja, tutatoka pamoja katika kuwavusha akina mama na watoto wakiwa salama” amesema Mhe. Telack.
Amesema sababu nyingi ni za mzaha na uzembe, mila potofu, uelewa mdogo wa wananchi pamoja na lishe duni.
Awali akitoa taarifa ya vifo vitokanavyo na uzazi katika Mkoa wa Shinyanga, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya katika Sekretarieti ya Mkoa wa Shinyanga Dkt. Rashid Mfaume, amesema kuwa, vituo 9 vya afya vipo katika hatua ya kukamilika ili vianze kutoa huduma za dharura za uzazi, ambapo Serikali ametoa jumla ya sh. bilioni 3.9.
Aidha, Dkt. Mfaume amesema kuwa, Serikali pia ametoa sh. Bilioni 3. Kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali mbili za Wilaya ya Ushetu na Shinyanga ili kupunguza tatizo la uhaba wa vituo vya Afya.
Kampeni hiyo ya Kitaifa iliyozinduliwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu, tarehe 6/11/2018 Mkoani Dodoma, inazinduliwa katika Mikoa yote nchini.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa