Katika kuhakikisha afya na ustawi wa mifugo, Halmashauri ya Manispaa ya Kahama kupitia Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Ushirika, imezindua kampeni kabambe ya utoaji wa chanjo na utambuzi wa mifugo, hatua inayolenga kuinua kipato cha mfugaji na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Kampeni hiyo, iliyoanza rasmi tarehe 19 Agosti 2024, ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Kitaifa wa utoaji wa huduma muhimu kwa mifugo, na itatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo hadi mwaka 2030.
Tayari, maelfu ya mifugo imepatiwa huduma muhimu huku wataalamu wa mifugo wakijipanga kuwafikia wafugaji wote nyumba kwa nyumba.
Miongoni mwa huduma zinazotolewa ni chanjo tatu muhimu ambazo ni Chanjo ya homa ya mapafu kwa ng’ombe ambapo mfugaji huchangia Shilingi 500 kwa kila ng’ombe; Chanjo ya sotoka kwa mbuzi na kondoo kwa kuchangia Shilingi 300 kwa mnyama na Chanjo ya kuku na bata mzinga inayotolewa bure kwa ajili ya kudhibiti milipuko ya magonjwa ya ndege.
Mpaka sasa, mafanikio makubwa yameripotiwa ambapo Ng’ombe 37,694, Mbuzi 4,215, Kondoo 513, Kuku 169,098 Bata mzinga 376 wamekwisha chanjwa.
Kwa ujumla, Kampeni hii si tu kwamba inalenga kupunguza vifo vya mifugo vinavyosababishwa na magonjwa, bali pia inalenga kuongeza tija kwa wafugaji, kuhakikisha mifugo ina afya bora na kuinua pato la familia kupitia uzalishaji ulioimarika.
Kwa Manispaa ya Kahama, huu ni mwanzo mpya wa mageuzi katika sekta ya mifugo na ni mfano halisi wa namna Serikali inavyoleta huduma karibu na wananchi kwa vitendo.
Mbali na chanjo, zoezi la utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni maalum linaendelea ambapo ng’ombe na punda huvalishwa hereni kubwa, huku mbuzi na kondoo wakivalishwa hereni ndogo. Utaratibu huu unasaidia kurahisisha ufuatiliaji wa afya, wizi wa mifugo, na kuweka kumbukumbu sahihi za mifugo katika maeneo yote ya Manispaa.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa mifugo kutoka Manispaa hiyo Pendo Matulanya amesema ratiba maalum imewekwa ili kuwafikia wafugaji wote bila kuwaacha nyuma.
Lengo ni kuhakikisha kila mnyama anapatiwa huduma stahiki bila kujali yupo kijijini au pembezoni mwa mji.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa