Kamishna wa Maadili, Sekretarieti ya Viongozi wa Umma, Jaji Mstaafu Harold Nsekela amefanya ziara Mkoani Shinyanga na kuzungumza na Viongozi wa Mkoa leo tarehe 19/06/2019 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ambapo amewakumbusha kufanya kazi kwa kuzingatia misingi bora ya Utumishi wa Umma pamoja na maadili.
Kikao hicho kilichoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack kimehusisha viongozi wa Mkoa, Wilaya ya Shinyanga pamoja na Taasisi za Umma.
Mhe. Nsekela amewataka viongozi wote kuhakikisha wanajaza fomu za uadilifu pamoja na tamko la mali za viongozi wa Umma kwa wakati na kwa uaminifu kwa sababu kazi ya Sekretarieti ya maadili ya viongozi ni pamoja na kuchunguza mwenendo wa utendaji kazi na kuwapeleka kwenye mamlaka za nidhamu viongozi wasio waadilifu.
Amesisitiza suala la mgongano wa kimaslahi katika utekelezaji wa majukumu ya Umma na kuwaonya viongozi kuepuka kutumia vibaya dhamana walizonazo kwa kutanguliza masilahi binafsi.
Awali akifungua kikao hicho,Mhe. Telack amesema suala la uadilifu kwa viongozi wa Umma ni muhimu sana katika kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Umma na pia kuongeza ubora katika maamuzi.
Telack amewataka viongozi katika Mkoa wa Shinyanga kumtanguliza na kumuogopa Mungu ili kuweza kusimamia wanayoyatekeleza kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu na kusimamia maendeleo ya nchi kwa usahihi.
Kamishna wa Maadili yupo katika ziara ya kuzungumza na viongozi wa Umma Mikoani ikiwa ni wiki ya maadhimisho ya Utumishi wa Umma inayofanyika kila mwaka kuanzia tarehe 16 - 23 Juni. Kauli mbiu ya maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma mwaka huu ni “Uhusiano kati ya Uwezeshaji wa vijana na usimamizi wa Masuala ya Uhamiaji,Kujenga Utamaduni wa Utawala Bora ,Matumizi ya TEHAMA na Ubunifu katika utoaji Huduma Jumuishi.”
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa