Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amezindua kampeni maalumu ya kupanda miti iliyopewa kauli mbiu ya "Shinyanga Mpya, Mti kwanza" yenye lengo la kuhakikisha Mkoa wa Shinyanga unakuwa na miti ili kuhifadhi mazingira na kurudisha hali ya Mkoa inayotishia kuwa jangwa.
Mhe. Telack amesema kuwa Mkoa wa Shinyanga ni kati ya maeneo yanayotajwa kuwa na jangwa, hivyo hali hiyo inayotaka kunyemelea na kuwa jangwa imesababishwa na wanashinyanga wenyewe.
"Jangwa linalotaka kunyemelea Mkoa wa Shinyanga tumelitengeneza sisi wenyewe, sasa tumeamua na kudhamiria, kwamba kwa mikono ileile ambayo ilitaka kuifanya Shinyanga iwe jangwa, sasa tuitumie kuhakikisha kwamba Shinyanga haiwi jangwa"
"Sasa tumedhamiria kuona kwamba Shinyanga inakuwa ya kijani, na inakuwa ya kijani kwa sisi kutumia nguvu zetu, kwa sisi kutumia umoja tulionao kuhakikisha tunapanda miti hii na kuisimamia kwa umoja wetu"amesema Mhe. Telack.
Ameagiza kila mmoja awe mlinzi wa mti kwa kila taasisi, kila nyumba kila mfanya biashara atapewa mti wa kutunza na atakayeshindwa atapelekwa mahakamani. Amesema ili kusimamia lazima kuwe na kutaratibu wa kuitunza kwa kuanza na Manispaa na hatimaye Mkoa mzima.
Kuhusu mifugo inayotembea ovyo na kuharibu miti, amesema kuanzia leo mfugo yoyote utakaokamatwa unazagaa ovyo faini ni shilingi elfu 50 kwa kila mfugo.
Kampeni hiyo iliyohudhuriwa na makundi mbalimbali ya wananchi wa Manispaa ya Shinyanga imeelezwa kuwa itakuwa endelevu kwani kila Taasisi, mwananchi, wafanyabiashara itapewa jukumu la kutunza miti iliyo kwenye maeneo yao.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Josephine Matiro amesema Kampeni hiyo ina lengo la kuhakikisha katika kila shughuli itakayofanyika lazima ianze kwa kupanda miti.
Amesema barabara zote ndani na nje ya Manispaa zitapandwa miti katika pande zote, aidha, kila mwananchi apande mti katika eneo lake. Amewahimiza wananchi kuwa watunzaji wa miti hiyo.
Mhe. Matiro amesema kuna utarativu mzuri uliowekwa ili kuhakikisha miti hiyo inatunzwa hususani kuiwekea fito na kufunga chupa kwa ajili ya kunyunyizia maji ili kudhibiti mifugo haribifu pamoja na kuweka watu maalum ambao watahakikisha miti inakuwa katika barabara zisizokuwa makazi ya watu.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa