Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Bw. Albert Msovela amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Shinyanga uwepo wa dawa za kutosha kwenye Hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya Mkoani hapa.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara Mjini Shinyanga, Bw. Msovela amesema hivi sasa, upatikanaji wa dawa katika Hospitali zote ndani ya Mkoa ni asilimia 80.
Amewahimiza wananchi kujiunga kwa wingi na mfuko wa Bima ya afya iliyoboreshwa (CHF) ili kuepuka gharama kubwa za matibabu kwani kwa mwaka mzima kaya moja yenye watu sita wanatibiwa wote kwa kulipia shilingi 10,000/= tu.
Msovela amewataka wananchi kutoa taarifa kwake au kwa Mganga Mkuu wa Mkoa iwapo watapata changamoto yoyote katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa pamoja na Vituo vya huduma za Afya kuhusu dawa au matibabu.
Kuhusu uhaba wa watumishi katika vituo vya kutolea huduma, Msovela amesema suala la upatikanaji wa watumishi linashughulikiwa na Serikali na tayari imeshaanza kutoa vibali vya ajira katika nafasi mbalimbali kwa ngazi zote hivyo wananchi wategemee kuona watumishi wakiongezeka japo si kwa kasi wanavyotarajia.
Akifunga mkutano huo wa hadhara uliokuwa na lengo la kusikiliza kero za wananchi, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amewataka wataalamu wote kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa zikiwa zimekamilika.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa