Kikao kazi cha uratibu wa utekelezaji wa Programu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM) kimefanyika mkoani Shinyanga kikihusisha wadau kutoka sekta ya afya, lishe, ustawi wa jamii, maendeleo ya jamii, elimu pamoja na shirika la ICS ambalo ni mdau kinara wa malezi ya watoto.
Kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga kimejadili kwa kina njia bora za kuhakikisha mtoto wa Kitanzania anapata msingi imara wa makuzi ya kimwili, kiakili, kihisia na kijamii tangu hatua za awali za maisha yake.
Miongoni mwa maazimio yaliyofikiwa ni kuhakikisha kila sekta inayohusika inakuwa na viashiria vya utekelezaji wa MMMAM ili kusaidia upatikanaji wa taarifa sahihi kwa kila robo mwaka. Pia, imependekezwa kuwa wataalamu wa sekta husika washiriki katika vikao vya kamati za wazazi na shule kwa lengo la kutoa elimu kuhusu malezi na makuzi kwa wazazi na walezi.
Aidha, kikao hicho kimehimiza kufanyika kwa vikao vya pamoja vya kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa MMMAM kutoka kila sekta kwenye ngazi ya mkoa. Ufuatiliaji wa ubora wa chakula cha watoto mashuleni pia umepewa kipaumbele, hasa kuhakikisha unga unaotumika mashuleni umetengenezwa kwa kiwango cha kurutubishwa.
Akizungumza katika kikao hicho, Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Shinyanga, Lydia Kwesigabo, amesema kuwa utekelezaji wa programu hii ni hatua muhimu kwa watoto kupata nafasi ya kukua kwa utimilifu katika nyanja zote za maisha yao. Alieleza kuwa ushahidi wa kisayansi unaonesha kuwa uwekezaji wa mapema kwa watoto huleta mafanikio ya muda mrefu katika afya, elimu na maendeleo ya jamii.
MMMAM ni moja ya mikakati inayotekelezwa kitaifa ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali na wadau katika kujenga kizazi chenye afya bora, maarifa na uwezo wa kuchangia maendeleo ya taifa.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa