Na. Paul Kasembo, SHY RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amesema kuwa kazi kubwa imefanywa na Serikali ili kuimarisha miundombinu ya barabara kwa Mkoa wa Shinyanga na nchi nzima kwani barabara nyingi zimefunguliwa na miradi mbalimbali ya miundombinu inaendelea kutekelezwa ambayo itakuwa na manufaa makubwa na hivyo kupunguza kero kwa wananchi.
RC Macha ameyasema haya leo Februari 26, 2025 akiwa kwenye kikao cha Bodi ya Barabara kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ambapo pamoja na yote amewataka Wakala ya Barabara Tanzania (TANROAD) na Wakala ya Barabara Vijijini (TARURA) mkoani Shinyanga kuhakikisha kingo za barabara zinazojengwa kwa kiwango cha lami zinakamilishwa kwa ubora unaotakiwa.
“Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kufanya kazi kubwa ili kuimarisha miundombinu ya barabara hapa mkoani Shinyanga na Nchi nzima kwa ujumla kwani mpaka sasa barabara nyingi zimefunguliwa maeneo mbalimbali, lakini pia miradi mbalimbali ya barabara inatekelezwa na itakuwa na manufaa makubwa sana kwa wananchi,” amesema RC Macha.
Akitolea mfano wa miundombinu inayotekelezwa mkoani Shinyanga, RC Macha amesema ujenzi wa barabara ya Kahama – Kakola pamoja na ujenzi wa madaraja Halmashauri ya Ushetu unaogharimu zaidi ya Tzs. Bilioni 18 ni vielelezo vikubwa vya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na miardi hii inategemewa kupunguza na kutatua kero za wananchi kuhusu miundombinu.
Aidha RC Macha amebainisha kuwa ujenzi wa barabara ya Ndala – Mwawaza inayoelekea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga yenye kilometa 4 inategemewa kupunguza kero kwa wananchi ambao wamekuwa wakihangaika kwa muda mrefu kutokana na ubovu wa barabara.
Kwa nyakati tofauti Kaimu Meneja wa TANROADS Mha. Joel Mwambungu na Kaimu Meneja wa TARURA Mha. Avith Theodory wamekiri kupokea ushauri, maelekezo na mapendekezo ya Bodi na kwamba wanakwenda kuyafanyia kazi kwa hataka na kwa weledi zaidi ili Serikali iweze kufikia lengo la kuwaboreshea miundombinu wananchi.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa