Naibu Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee, Wanawake na Watoto Mhe. Dkt. Hamis Kigwangala amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Sihaba Nkinga kukamilisha taratibu za kuhamisha makazi yote ya wazee nchini kuwa chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI ambayo kimsingi ndiyo yenye jukumu la kuendesha makazi ya wazee hao kwa sababu wako karibu kwa maana ya Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mhe. Kigwangala ametoa agizo hilo hivi karibuni katika ziara yake ya siku moja Mkoani hapa ambapo ametembelea makazi ya wazee katika kambi ya Kolandoto, Manispaa ya Shinyanga.
Amesema, Wizara ya Afya itaendelea na jukumu la kutoa Sera na miongozo ya kuwahudumia Wazee hao na Mamlaka za Serikali za Mitaa yaani Halmashauri za Wilaya, Manispaa, Miji na Majiji ndiyo zenye jukumu la kuendesha makazi na vituo hivyo kwani ndiyo wako karibu na wazee.
Aidha, amemuelekeza Katibu Mkuu wa Afya awasiliane na Katibu Mkuu TAMISEMI ili kujenga vituo 10 kwenye Mikoa ambayo haina vituo vya Wazee, ikiwa ni hatua ya awali ya kila Mkoa kuwa na Makazi ya Wazee, ambapo hadi sasa kuna vituo 17 nchi nzima vyenye wazee 459.
Hata hivyo Mhe. Kigwangala amesema kuwa, kwa mujibu wa sera sehemu ya kwanza ya wazee kutunzwa ni ndani ya familia na Serikali huchukua jukumu hilo baada ya ngazi zote kushindwa kuwatunza, hivyo ametoa rai kwa wananchi wote kuhakikisha wanawatunza wazee kuanzia kwenye familia zao.
"Ni muhimu kuzingatia tamko la sera, kuwatunza ni jukumu la familia hivyo tusiwanyanyapae sababu ya umri wao, tuwashirikishe kwani ni tunu kubwa" amesisitiza Mhe. Kigwangala.
Kigwangala amewataka wananchi kukemea vitendo vya ukatili kwa wazee na kuondoa vikwazo vinavyowakosesha amani na kuwa, Serikali itaendelea kuchukua hatua kali kwa wale wote watakaobainika wanafanya vitendo vya ukatili kwa wazee.
Katika ziara hiyo, Mhe. Kigwangala ameweka jiwe la msingi ujenzi wa bweni la wazee ambalo litakuwa na uwezo wa kubeba wazee 20, amekabidhi bajaji itakayowasaidia wazee hao usafiri wa karibu pia amefungua jiko maalumu litakalotumika kupikia wazee likiwa na majiko ya gesi.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa