Na. Paul Kasembo, SHY RS.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amepiga marufuku kwa yeyote ambaye ni mhamiaji haramu kujiandikisha katika Orodha ya Daftari la Wapiga Kura mkoani Shinyanga na kuiagiza Kamati ya Usalama na Idara ya Uhamiaji kuhakikisha (wasiotambulika kisheria) kutoka nchi za jirani hawapati nafasi hiyo kwa lengo la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika tarehe 27 Novemba, 2024 kwani wao si wakazi halali nchini hii kisheria.
RC Macha ameyasema haya leo tarehe 12 Oktoba, 2024 wakati akijiandikisha katika daftari la wapiga kura kwenye Kata ya Lubaga iliyopo hapa Manispaa ya Shinyanga huku akiwa ameongozana na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Julius Mtatiro (Wakili), Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Mwl. Alexius Kagunze, Msimamizi wa Uchaguzi Mkoa wa Shinyanga ndg. Bakari Kasinyo na watumishi wandamizi wengine kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Manispaa.
Katika kuelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao utafanyika mwezi Novemba, 2024, Mkoa wa Shinyanga unatarajiwa kuwa na wapiga kura 1,158,025 ambapo Manispaa ya Shinyanga inao jumla ya wapiga kura 126,345, Manispaa ya Kahama 253,078, Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu 168,005, Msalala 189,492, Shinyanga 236,621 pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu wapiga kura 184,484.
Ikumbukwe kuwa, Mkoa wa Shinyanga una Mitaa 90, Vijiji 506, Vitongoji 2007 pamoja na Vituo vya kujiandikisha wapiga kura 2,897 huku wito na msisitizo ukitolewa kwa wananchi kutumia fursa na haki yao ya kimsingi ya kugombea nafasi hizo na kushiriki kikamilifu kwenye Uchaguzi huu katika maeneo wanayoishi.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa