Afisa Elimu wa Mkoa wa Shinyanga, Samson Allute Hango ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa mfumo wa Ujifunzaji wa Umahiri kwa Njia ya Sauti (AICBL), amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuhitaji walimu wabunifu wanaobuni mbinu na zana zitakazowasaidia wanafunzi kuelewa kwa urahisi.
Amesisitiza kuwa ubunifu wa walimu ni nyenzo muhimu katika kuongeza umahiri wa wanafunzi na kuinua matokeo ya kielimu.
Uzinduzi huo umefanyika Septemba 30, 2025 katika Shule ya Sekondari ya Wavulana Shinyanga iliyoko Wilayani Kishapu, ambapo Hango amempongeza Mwalimu David Ipamba, Mratibu na Mbunifu wa maabara ya Jiografia shuleni hapo, pamoja na wanafunzi walioshiriki katika ubunifu huo.
Ameeleza kuwa ushirikiano baina ya walimu na wanafunzi ni msingi wa mafanikio ya kitaaluma, akitaja kuwa shule hiyo inapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa shule zote za Mkoa wa Shinyanga.
Mwl. David Ipamba ameeleza kuwa mfumo wa AICBL umeundwa kwa lengo la kutumia sauti, modeli, na mbinu za vitendo ili kujenga mazingira shirikishi ya ujifunzaji. Mfumo huo unawajengea wanafunzi uwezo wa kufikiri kwa kina, kubuni, na kujenga stadi za karne ya 21 kama vile ubunifu, mawasiliano na ushirikiano. AICBL pia inalenga kuwafikia wanafunzi wote, wakiwemo wenye mahitaji maalum, kupitia matumizi ya redio, simu, na vifaa vya TEHAMA.
Mwakilishi wa Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Kishapu, Moshi Moshi, amepongeza jitihada hizo na kutoa wito wa kuendelea kuboresha vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Kwa upande wake, Mkuu wa Shule hiyo, Mwl. Bernard Ishengoma, amesema shule yao imejipanga kuongeza ubunifu, kusimamia nidhamu, na kuhakikisha kila mwanafunzi anashiriki kikamilifu katika masomo na shughuli za kuendeleza ujuzi.
Shule ya Sekondari ya Wavulana Shinyanga, iliyoanzishwa mwaka 1966, kwa sasa ina jumla ya wanafunzi 930 wakiwemo 118 wenye mahitaji maalum. Kupitia mfumo wa AICBL, shule hiyo inalenga kuwa kitovu cha ubunifu na ubora wa elimu si tu kwa Mkoa wa Shinyanga bali kwa Tanzania nzima.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa