Na. Paul Kasembo, SHY RS.
NAIBU Waziri wa Maji Mhe. Eng. Mathew Kundo (MB) akiwa ameambatana na watalaam mbalimbali amemtembelea ofisini kwake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha ambapo pamoja na mambo mengine pia amemueleza dhamira ya ziara yake mkoani Shinyanga ambapo ametembelea na kukagua mradi wa Maji ya Ziwa Victoria katika chanzo cha maji kilichopo Ihelele Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.
Kisha baadae kukagua mradi wa maji unaotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Kishapu hapa Shinyanga ambapo pia alihutubia wananchi kupitia mkutano wa hadhara ambao ulihudhuriwa na Mbunge wa Jimbo la Kishapu Mhe. Boniphace Butondo na wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Maji na baadhi ya wakuu wa Taasisi kutoka Shinyanga.
"Nimefika hapa kukusalimu na kukueleza kuwa nimekuwa hapa tangu jana ambapo nimetembelea na kukagua miradi mbalimbali ukiwemo wa Maji ya Ziwa Victoria ambao unatekeleza shughuli zake kutoka katika chanzo cha maji cha Ihelele Mwanza na baadae nilifika Kishapu kwenye mradi wa RUWASA, kisha niliongea na wananchi kupitia mkutano wa hadhara pale Uchunga, na leo nitafanya kikao na watumishi wa Mamlaka za Maji hapo baadae," amesema Mhe. Kundo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amemueleza Mhe. Kundo kuwa, mradi wa maji ya Ziwa Victoria unaotoa huduma ya maji kwa Mamlaka nyingine za maji hapa Shinyanga unatekelezwa vema sana huku akieleza uwepi wa baadhi ya changamoto ambazo huikabili KASHWASA ikiwa ni pamoja na inapojitokeza changamoto za kiufundi na upungufu wa nishati ya umeme jambo ambalo hupelekea upungufu wa utoaji huduma ya maji kwa baadhi ya maeneo mkoani Shinyanga.
Pia RC Macha amezungumzia pia uwepo wa baadhi ya Taasisi ambazo zimekuwa zikilipa ankara kwa kusuasua jambo ambalo linakwamisha utoaji wa huduma tarajiwa kwa wananchi kwani zimekuwa na malimbikizo ya madeni ya muda mrefu huku akisema kuwa yeye mwenyewe amekwishachukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kuziita hizo taasisi na kuziagiza kulipa madeni hayo kwa wakati.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa