Na. Paul Kasembo, Ihelele Mwz.
NAIBU Waziri wa Maji Mhe. Eng. Mathew Kundo amesema kuwa ameridhishwa sana na utekelezaji wa Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria ambao chanzo chake ni Ihelele Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza unaosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama Shinyanga (Kahama Shinyanga Water Supply and Sanitation Authority - KASHWASA) iliyopewa jukumu kuu la kuzalisha, kusambaza na kuuza maji jumla kwa Mamlaka zingine zinazohusika na usambazaji wa maji kwa wananchi katika Mikoa 6 ikiwemo Shinyanga, Geita, Simiyu, Tabora, Mwanza na Singida.
Mhe. Kundo ameyasema haya alipotembelea na kukagua chanzo hiki cha maji ambacho kinatajwa kuwa mkombozi wa huduma ya maji ambacho kinawafikia wananchi katika maeneo mengi zaidi ya mijini na vijijini huku akimpongeza sana Mkurugenzi wa KASHWASA Mhandisi Patrick Nzamba kwa utekelezaji wake mzuri wa kazi yeye na wasaidizi wake ambao umekusudia kuhakikisha kuwa huduma ya maji inawafikia wananchi walio wengi huku akitolea mfano wa utiaji saini wa zaidi ya Bil 600 upelekaji maji Kishapu wilayani Kahama.
"Niwapongeze sana KASHWASA kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuwahudumia wananchi katika miji na vijiji kwa Mikoa 6, hii ni kazi nzuri sana kwa wananchi wetu na ndiyo maelekezo ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa na huduma ya maji safi na salama wakati wote. Na katika hili nitoe wito kwa wananchi wote kutunza vyanzo vyote vya maji pamoja na miundombinu yake ili iendelee kuwanufaisha na vizazi vijavyo," amesema na kusisitiza Mhe. Kundo.
Baadae Mhe. Kundo ametembelea Tangi kubwa la kuhifadhi maji lenye ujazo wa Lita Mil. 35 lililopo Mabale ambalo hutumika kupeleka maji katika maeneo yote yanayohudumiwa na KASHWASA huku Mhandisi Nzamba akisema kuwa chanzo cha Ihelele chenye uwezo wa kuzalisha maji Lita Mil. 80 kwa siku kinaouwezo wa kufanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa zaidi na kukidhi mahitaji ya wananchi iwapo haitokei changamoto ya kiufundi au inayohusu nishati ya umeme.
HABARI PICHA
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa