Na. Shinyanga RS
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa (MB) leo tarehe 4 Desemba, 2023 amefika Mkoani Shinyanga na kufanya kikao na watumishi wa Sekta ya Ardhi ambapo pia alipewa taarifa ya Utekelezaji wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri Mkoa wa Shinyanga kuhusu utatuzi wa Migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975, na kupongeza sana namna ambavyo imetekelezwa.
Hayo yamesemwa leo na Mhe. Silaa katika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi ya mkuu wa mkoa wa shinyanga na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo mkuu wa mkoa wa shinyanga Mhe. Christina Mndeme, Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Prof. Siza Tumbo, mkuu wa wilaya ya Kahama Mhe. Mboni Mhita.
Pia aliambatana na mwenyeviti wa Halmashauri ya wilaya ya shinyanga, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Shinyanga Ndg. Leo Komba, wakurugenzi wa Halmashauri zote na watumishi mbalimbali wa sekta ya ardhi huku akiwataka watumishi wote wa ardhi kubadilika katika utendaji kazi wao wa kila siku.
"Niwapongeze sana Mkoa wa Shinyanga kwa utekelezaji huu mzuri wa maelekezo ya Baraza la Mawaziri, mmefanya kazi nzuri sana hivyo ni wajibu wa sasa wa kila mtumishi wa sekta ya ardhi kubadilika katika utendaji kazi wa kila siku ili kusiwepo na kero za ardhi tena", alisema Mhe. Silaa.
Awali akimkaribisha Mhe. Silaa, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme alisema kuwa ifike wakati sasa ardhi iwe ni baraka na siyo laana kwetu. Mhe. Mndeme aliendelea kumueleza Mhe. Silaa kuwa, mkoa wa shinyanga unaendeleaza utatuzi wa migogoro ya ardhi, kusimamia matumizi bora ya ardhi na kwenye ile migogoro mikubwa mkoa utaomba msaada kwake waziri mwenye dhamana ili aweze kusaidia.
Akitoa salamu za Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Mhe. Ngassa Mboje ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo alisema, kumekuwa na baadhi ya migogoro sugu katika eneo la Nyanhwale na Halmashauri ya Wilaya ya Geita kupitia kijiji cha Chang'ombe ambapo Halmashauri ya Wilaya Geita wamekuwa wakidai ni eneo lao. Kufuatia malalamiko hayo Mhe. Silaa alimuelekeza Katibu Mkuu na Msajili wa Mabaraza kufika Shinyanga kutatua kero hizo.
HABARI PICHA
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa