Na. Shinyanga RS.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesaini Mkataba wa kuzalisha UMEME WA JUA kwa kutumia Teknolojia ya SOLAR PHOTO VOLTAIC wenye uwezo wa kuzalisha MEGAWATI 150 ambapo itatekelezwa kwa awamu mbili, awamu ya kwanza megawati 50 na kisha megawati 100 utajengwa katika Kijiji cha Ngunga, Kata ya Talaga Wilaya ya Kishapu Mkoa wa Shinyanga mradi unaotajwa kuwa mkubwa zaidi kuwahi kutokea hapa nchini na katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo, Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba alisema kuwa kusainiwa kwa mradi huu ni sehemu ya mipango ya mapinduzi katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo mseto katika Sekta ya Nishati nchini ili kuweza kufikia lengo la kuwa na megawati 5000 kwenye Gridi ya Taifa ifikapo 2025.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme ambaye ndiye mwenyeji wa mradi huo katika Mkoa huo alimshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Munngano wa Tanzania, Wizara ya Nishati na Tanesco kwa kuwezesha utiaji saini wa mradi huo muhimu zaidi ambao utakwenda kuinufaisha Shinyanga kwa kuzalisha nishati, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi wa wananchi kwa ujumla.
"Kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Shinyanga, napenda kutoa shukurani zangu za dhati kabisa kipekee kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wizara ya Nishati na Tanesco kwa kuwesesha utiaji saini wa mkataba huu leo, hii ni furaha sana kwetu kwakuwa pamoja na kuzalisha umeme lakini pia mradi unakwenda kuongeza ajira na kuinua uchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na pato la Taifa kwa ujumla," alisema Mhe. Mndeme.
Hafla ya utiaji saini wa mkataba wa kuzalisha umeme kwa teknolojia ya SOLAR PHOTO VOLTAIC imeongozwa na Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Mhe. Christina Mndeme ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Kaimu Mwenyekiti Kamati ya Nishati na Madini ya Kudumu ya Bunge Mhe. Judith Kapinga, Mhe. Boniphace Butondo Mbunge Jimbo la Kishapu, wakandarasi kutoka Kampuni ya CHICO na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba akielezea jambo wakati wa utiaji saini wa mkataba
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme akiongea jambo wakati wa utiaji saini
Picha ikionesha viongozi mbalimbali wakishuhudia utiaji saini wa mkataba wa uzalishaji wa umeme wa jua
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa