Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amekabidhi misaada yenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 2 kwa wanawake 23 wahitaji wanaoishi katika Tarafa ya Ibadakuli, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.
Mhe. Telack amekabidhi misaada hiyo ambayo imetolewa na wahisani mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambayo kimkoa yamefanyika katika viwanja vya shule ya msingi Ibadakuli mapema jana.
Akitoa shukrani kwa Mhe. Mkuu wa Mkoa, kwa niaba ya wanawake wa Ibadakuli, mmoja wa wanawake hao Bibi Maria Kapela amesema kuwa, wanawake wengi hasa wanaofanya kazi kwenye baadhi ya viwanda, wanashindwa kutimiza malengo yao ya kiuchumi kutokana na ujira mdogo wanapata viwandani.
Aidha, wamemueleza kuwa wana changamoto ya kutokuwa na eneo maalum la kuuzia bidhaa zao hivyo wamemuomba awasaidie kupata eneo hilo katika Manispaa ya Shinyanga.
Akizungumza na wanawake pamoja na wananchi kwa ujumla, Mhe. Telack amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga kutafuta eneo ambalo kina mama wajasiriamali wataweza kuuza bidhaa ili waendelee kuzalisha na wapewe maelekezo jinsi ya kuweza kupata eneo.
Mhe. Telack pia amemuagiza Afisa kazi Mkoa, kufahamu idadi ya wanawake wanaofanya kazi viwandani na kwenda kwenye viwanda kuzungumza na wamiliki wa viwanda kuhusu maslahi ya wanawake wanaofanya kazi viwandani na kuwasilisha taarifa kwake.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa