Na. Shinyanga RC.
KATIBU Msaidizi, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Magharibi Ndg Gerald Mwaitebele ametoa mafunzo haya kwa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA Mkoa wa Shinyanga huku akiwataka kuanzia sasa kuyaishi maadili haya kwakuwa wao ni watumishi wa umma na kwamba ni kioo kwa umma wanaoutumikia.
Maelekezo haya yanetolewa leo na Mwaitebele katika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi za mamlaka hii mbele ya watumishi wote huku akiwasisitiza kubadilisha tabia, matumizi mabaya ya lugha kwa wanaowahudumia, kuacha kuomba rushwa, kukopa bila kuoipa, kutoa siri za ofisi ili kuihujumu na badala yake wawe waadilifu ndani na nje ya ofisi kwakuwa wao ni viongozi wa umma.
"Kuanzia sasa tubadilishe mwenendo wetu, tubadili tabia zetu, matumizi ya lugha kwa tunaowahudumia ambao ndiyo umma, tuanze kuyaishi maadili kuanzia leo na tukumbuke kuwa sisi ni viongozi tunaotumikia umma hivyo tunatakiwa kuwa kioo mbele ya umma", alisema Mwaitebele.
Kando na hayo Mwaitebele alitaja miongoni mwa sifa na utambulisho wa mtumishi mwadilifu kwa umma ikiwemo na kujali wengine, kujitolea kusaidia wenye uhitaji, kuwa msikivu, mwaminifu nyakati zote na anayeheshimu kila mtu bila ubaguzi. Sifa nyingine ni pamoja na kuwa mnyenyekevu, kufanya kazi kwa bidii, kutenda haki, anapaswa kufikiria kwa makini kabla ya kutenda, kujizuia na tamaa ya aina yoyote na kuwa tayari na kukubali kukoselewa na kubadilika.
Misingi ya maadili katika Sekta ya umma ni muhimu sana ili kulinda maslahi ya umma na kukuza uwajibikaji kwa umma, sheria ya maadili ya viongozi wa umma, sheria ya utumishi wa umma pamoja na kanuni zake zimeanisha misinhi kadhaa ikiwemo Uadilifu, Haki ya kutopendelea, Kuheshimu sheria, kutopokea zawadi au fadhila kutoka kwa unayemuhudumia.
Awali akimkaribisha muwezeshaji, Meneja TRA Mkoa wa Shinyanga Ndg. Faustine C. Mdessa alisema kuwa wao kama watumishi na viongozi wa umma wapo tayari kupokea mafunzo ya maadili ya viongozi wa umma, wapo tayari kupokea maelekezo, miongozo na ushauri wote watakaopewa na kwamba kuanzia sasa wamebadilika na watayaishi.
Picha juu ikimuonesha Ndg. Gerald Mwaitebele, Katibu Msaidizi, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kanda ya Magharibi akielezea jambo wakati wa mafunzo.
Picha juu ikimuonesha Ndg. Faustine Mdessa Meneja TRA Mkoa wa Shinyanga
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa