Na: Paul Kasembo.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha, ametoa wito kwa vijana mkoani hapa kutathmini upya mbinu wanazotumia katika kujipatia kipato, kwa kuzingatia usalama wao, uhalali wa shughuli hizo pamoja na mustakabali wa maisha yao ya sasa na baadae.
Akizungumza na vyombo vya habari kufuatia tukio la ajali ya mgodi wa dhahabu namba nane (8) katika Kata ya Mwakitolyo, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Mhe. Macha alisema kuwa ofisi yake iko wazi kupokea na kufanyia kazi ushauri wowote kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu tukio hilo. Alisisitiza kuwa hadi sasa Serikali imethibitisha vifo vya watu sita (6) na majeruhi kumi na mmoja (11), ambapo wanne kati yao tayari wameruhusiwa kutoka hospitali, mmoja amehamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, wawili wanaendelea kupatiwa matibabu katika wodi na wengine watatu walipokelewa na kuhudumiwa katika Zahanati ya Mwakitolyo.
“Nitumie nafasi hii kutoa wito kwa vijana wote hapa Shinyanga kutathmini kwa kina njia wanazotumia kujipatia kipato. Kuna mifano mizuri ya vijana wanaojihusisha na kilimo cha kisasa na kufanikiwa. Mathalani, vijana wa Kikundi cha Jipange kilichopo Kata ya Kishapu wanajishughulisha na kilimo cha matunda kama tikiti maji na Kata ya Songwa wanaojishughulisha na kilimo cha nyanya na mpunga. Hawa ni baadhi tu ya vijana na vikundi vya kuigwa kwani wameweza kuinua maisha yao kiuchumi kwa kutumia njia salama na halali,” alisema Mhe. Macha.
Aidha, RC. Macha alisisitiza kuwa taarifa rasmi kuhusu ajali ya mgodi huo alizitoa akiwa eneo la tukio husika (ndani ya mgodi) na leo tena alirejea mbele ya wanahabari na pia alikanusha uvumi ulioenea kupitia baadhi ya vyombo vya habari kuhusu idadi tofauti ya waliofukiwa mgodini na kwamba hofu ilitanda eneo hilo kuwa siyo za kweli kabisa.
Ajali hiyo iliripotiwa kutokea mnamo Mei 17, 2025 majira ya saa 5 asubuhi katika mgodi huo wa dhahabu uliopo Mwakitolyo, ambapo hatua mbalimbali zimechukuliwa kuhakikisha wahanga wanapata huduma stahiki na kuchunguzwa kwa kina ili tukio kama hilo lisijirudie tena.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa