Na. Paul Kasembo, KISHAPU DC.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amesema kuwa ameridhishwa na kasi inayoendelea katika kilimo cha zao la pamba huku akiwasisitiza wataalamu kuendelea kuwafikia wakulima katika maeneo yao na kuwaelimisha matumizi ya vifaa vya kisasa ikiwemo ndege ndogo zisizokuwa na rubani (drone) katika kuboresha zao hili ambapo zinatumika kunyunyizia dawa shambani, ndege ambazo zimepelekwa na Bodi ya Pamba.
Hayo ameyasema wakati akifanya ukaguzi, hamasa na ufuatiliaji wa kilimo cha zao la pamba wilayani Kishapu ambapo pamoja na mambo mengine RC Macha amesema kuwa uwepo wa vifaa hivyo vya kisasa unamuwezesha mkulima kunyunyizia dawa katika shamba lenye ukubwa wa Hekari 1 kwa dakika 6 tu, jambo ambalo linatajwa kuwa mkombozi mkubwa wa mkulima wa zao la pamba.
"Nimefuatilia na kukagua mashamba yenu ndugu zangu niseme kuwa nimeridhishwa sana na kasi ya kilimo cha zao hili la pamba hapa wilayani Kishapu, hakika sasa tunakwenda kurejesha heshima ya zao la pamba kama ilivyokuwa hapo awali na hili ndiyo kusudio la Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha kilimo hiki cha pamba kinakuwa ni chenye tija zaidi kwenu na kuchechemua uchumi wa wananchi pamoja na kuongeza pato la Taifa," amesema RC Macha.
RC Macha akiwa ameongozana na mwenyeji wake Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Peter Masindi, Katibu Tawala Wilaya ya Kishapu Bi. Fatma Mohamed, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kishapu Ndg. Emmanuel Johnson na wataalamu wengine ambapo amesisitiza kuwa, lengo la Serikali ni kuona kila mkulima wa zao la pamba anahakikisha kuwa kila Hekari moja (1) inazalisha kuanzia Kilo 1000 hadi 1200.
Kiwango hicho kinatajwa kuwahi kufikiwa hapo awali ambapo walikuwa wanafikia hadi Kilo 1800 kwa hekari 1 na hivyo kukifanya kilimo cha zao la pamba kuwa ni moja kati zao la biashara na yenye tija zaidi kwa wananchi mkoani Shinyanga na kustawisha maisha yao.
Huu ni mwendelezo wa ziara za RC Macha za kuwafikia wananchi moja kwa moja katika maeneo yao ikiwemo shambani akiwa na lengo la kuhakikisha amesikiliza na kutatua changamoto zao.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa