Na. Paul Kasembo, SHY RS.
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Shinyanga SACP Janeth S. Magomi amesema kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga Kikosi cha Usalama Barabarani limekagua, kubaini na kukamata jumla ya makosa 6320 ya Usalama Barabarani ambapo makosa 4847 ni ya magari, 1473 ya pikipiki na bajaji huku wahusika wakiwajibishwa kwa kulipa.
RPC Janeth ameyasema haya leo tarehe 27 Mei, 2024 alipokuwa akitoa Taarifa kwa Umma ambayo inaonesha kuwa makosa haya yamepatikana kati ya Aprili 17, 2024 na Mei 27, 2024 huku akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga litaendelea kuimarisha ulinzi na usalama kwa kushirikiana na Jamii katika kubaini na kutanzua uhalifu kwa kufanya doria, misako pamoja na oparesheni mbalimbali katika kufanikisha kazi zake.
"Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani limefanya ukaguzi mbalimbali na kubaini jumla ya makosa 6320 ikiwa 4847 ni kutoka katika magari na 1473 ni kwenye pikipiki na bajaji ambapo wahusika wamewajibishwa kwa kulipa faini za papo kwa hapo," amesema RPC Janeth.
Wito umetolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kwa wananchi wote kuendelea kushirikiana na Polisi katika kubaini na kutanzua uhalifu wa kijinai ikiwemo usafirishaji, uuzaji na utunzaji wa dawa za kulevya na kwamba, Polisi haitasita kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria kwa yeyote yule atakayekiuka sheria za nchi.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa