Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako ameyasema hayo leo tarehe 10/11/2019 katika hafla ya kupokea vyumba vinne vya madarasa kutoka kwa umoja wa Wake wa Viongozi - New Millenium Women Group, katika shule ya msingi Buhangija vilivyojengwa kwa shilingi milioni 16.4 kila chumba chini ya usimamizi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
"Wengine wakipewa fedha hiyo wanasema haitoshi, lakini hapa imetosha na kubaki, nawapongeza sana. Nawasihi wale wanaosema mil. 20 haitoshi kujenga darasa waje Shinyanga kujifunza"
Amewapongeza na kuwashukuru Wake wa Viongozi kwa kazi hiyo ya ujenzi wa madarasa na kusema kuwa wamefanya kazi ya kuunga mkono kwa vitendo jitihada za Serikali ya awamu ya tano kwani Serikali inafanya kazi kubwa lakini pia mahitaji ni makubwa.
Aidha, amewasisitiza Watanzania wote kuacha tabia ya kuwanyanyapaa watoto wenye ulemavu wa namna yoyote, kwani wana haki ya kupata elimu na kutimiza ndoto zao.
Akikabidhi madarasa hayo pamoja na matundu 10 ya vyoo, mlezi wa umoja wa wake wa viongozi Mama Mary Majaliwa ameupongeza uongozi wa Mkoa kwa kusimamia vizuri ujenzi huo na kuongeza umoja huo unaongeza sh. Mil 3.6 kwa ajili ya madawati.
Akitoa taarifa ya ujenzi huo Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Bw. Albert Msovela amesema, Mkoa ulipokea sh. Mil. 92 iliyotolewa na Umoja huo kwa awamu tatu na kukamilisha vyumba vyote vinne vya madarasa kwa sh. mil. 65.8 pamoja na matundu 10 ya vyoo yanayotarajiwa kukamilika mwezi ujao kwa gharama ya sh. mil .26.2
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack ametoa shukrani za dhati kwa umoja huo wake wa Viongozi na kuwaomba waendelee kuguswa kuwasaidia watoto hao wa shule ya msingi Buhangija ambayo ni shule inayojumuisha na watoto wenye mahitaji maalum.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa