Na. Shinyanga RS.
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Pro. Siza D. Tumbo amefunga kambi ya michezo na kuwatakia ushindi timu ya UMITASHUMTA mkoa wa Shinyanga katika mashindano yao Kitaifa wanayokwenda kushiriki katika Manispaa ya Tabora Mkoa wa Tabora.
Pro. Siza ameyasema hayo leo tarehe 1 Juni, 2023 wakati wa alipokuwa akizungumza na timu ya wanamichezo wa UMITASHUMTA katika ukumbi wa mikutano uliopo Chuo cha Ualimu Shinyanga (SHYCOM) huku akisisitiza kuwa ili warudi na ushindi wanapaswa washindane kwa umakini, bidii, maarifa na nidhamu wakati wote watakapokuwa katika mashindano hayo.
“Rai yangu kwenu wanangu, wanamichezo na wawakilishi wa Mkoa wetu kwenda kushindana kwa bidii, maarifa na nidhamu kubwa wakati wote huku mkizingatia kuwa Mkoa umewaamini na ndiyo maana kati ya wengi mmechaguliwa ninyi kutuwakilisha, na katika hili niseme tu kwamba Serikali ya Mkoa wa Shinyanga ipo nanyi wakati wote na mimi binafsi ni muumini wa michezo kwakuwa najua michezo ni zaidi ya burudani, michezo ni afya, ni undugu na kikubwa michezo ni ajira kama zilivyo ajira nyingine,” alisema Pro. Siza.
Pro. Siza alitumia fursa hiyo kuwaeleza walimu katika shule zote Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha kuwa wanakuwa na vipaumbele vya michezo katika shule zao zote za Msingi na Sekondari kama ambavyo imeoneshwa kwenye program ya uendeshaji wa michezo na utamaduni ambayo inaonesha kila siku kutakuwa na muda maalumu kwa ajili ya michezo, sanaa na utamaduni huku akiwataka kupanda mbegu za michezo za muda mrefu ili baada ya miaka mitano ijayo Shinyanga iwe ya mfano.
Akisoma taarifa ya mashindano ya michezo Mkoa wa Shinyanga kwa mwaka 2023 Mwalimu Mayasa Mwinyijuma alisema kuwa, kambi ya UMITASHUMTA 2023 Mkoa wa Shinyanga ilianza mara baada ya mashindano ya Halmashauri kukamilika tarehe 22 Mei, 2023 ambapo alieleza kabla ya ngazi ya Mkoa mashindano hayo yalifanyika ngazi ya shule, kata, kanda na Wilaya ili kupata timu za Wilaya.
Timu ya UMITASHUMTA MKoa wa Shinyanga imeondoka kuelekea Manispaa ya Tabora Mkoani Tabora na wanafunzi 120, walimu wa michezo 14 na daktari wa michezo 1.
Picha ya pamoja ikionesha baadhi ya washiriki, walimu na viongozi mbalimbali baada ya kufunga kambi ya michezo.
Muonekano wa Bango lenye kauli mbiu likiwakilisha UMITASHUMTA Mkoa wa Shinyanga.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa