Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Profesa Joyce Ndalichako amemtaka Mkandarasi wa ujenzi na ukarabati katika chuo cha ualimu Shinyanga kampuni ya “Afrique Co. Ltd” kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja anakamilisha kazi zote anazotakiwa kutekeleza kwani ameshalipwa karibu fedha yote lakini kasi yake hairidhishi.
Prof. Ndalichako pia amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kumuondoa mara moja Mkuu wa chuo cha Ualimu Shinyanga (Shycom) na kumtaka Mkurugenzi wa Taasisi ya kupambana na kuzuia Rushwa TAKUKURU kuanza kufanya uchunguzi wa mwenendo wa manunuzi katika mradi wa upanuzi na ukarabati wa majengo katika chuo hicho.
Ndalichako ametoa agizo hilo mapema leo tarehe 05 Oktoba, 2018 alipotembelea chuo hicho cha Ualimu kukagua maendeleo ya mradi wa upanuzi na ukarabati wa majengo unaogharimu Serikali sh. Bilioni 9.4 na kuzungumza na wanafunzi pamoja na wakufunzi.
Amesema amesikitishwa na kushangazwa na kasi ndogo ya kiwango cha ujenzi ambapo Mkandarasi huyo ameshalipa jumla ya sh. bil. 2.7 pamoja na kitendo cha Mkuu wa Chuo kumsifia kuwa anafanya vizuri wakati Mkandarasi mshauri wa mradi ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo kikuu cha Ardhi Profesa Evaristo Liwa amesema hakuridhika na mwenendo wa mkandarasi huyo tangu mwanzo.
Kwa mujibu wa taarifa ya mshauri huyo, mkandarasi alishapewa onyo mara tatu na alishauri Wizara ivunje naye mkataba lakini cha ajabu Wizara imemlipa tena mkandarasi huyo sh. bilioni 244 tarehe 02 Oktoba ambapo Ndalichako amesema, maafisa Elimu pia wa Wizara yake wachunguzwe.
Aidha amemtaka pia mkandarasi wa pili katika mradi huo kampuni ya Masasi Construction kukamilisha kazi zake maramoja kwani na yeye mkataba umeisha muda wake.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko ameahidi atafuatilia na kumsimamia mkandarasi kuhakikisha kazi zote zinakamilika ndani ya mwezi mmoja na kumpa taarifa Waziri.
Mradi huo wa ujenzi, upanuzi na ukarabati wa majengo unaotekelezwa na Serikali katika vyuo vinne vya ualimu nchini nzima ikiwemo chuo cha Ualimu Shinyanga, una thamani ya zaidi ya sh. Bilioni 36.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa