Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack amekabidhi Pikipiki 14 kwa Maafisa Tarafa wa Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi wao na kuonya kuwa hatarajii kuona pikipiki hizo zikitumika nje ya shughuli za Serikali.
Kiongozi huyo wa Mkoa wa Shinyanga amekabidhi pikipiki hizo kwa niaba ya Rais John Pombe Magufuli na kuwataka maafisa tarafa hao kuhakikisha pikipiki hizo zinatunzwa vizuri ili wengine waweze kuzitumia na kuwaonya watendaji hao kutotumia pikipiki hizo kubeba abiria kama ilivyo kwa madereva bodaboda.
Aidha Bi. Telack amewataka Maafisa Tarafa hao pamoja na kupewa pikipiki mpya pia wahakikishe wanatunza Ofisi walizojengewa pamoja na vifaa walivyopewa kwa lengo kuwezesha mazingira mazuri ya utendaji kazi zinatunzwa vizuri akionya kuwa baadhi yao tayari washaanza matumizi mabaya ya vifaa hivyo.
‘’Wapo watu wanafanya vizuri na tumeanza kuona mnavyofanya kazi vizuri, yapo matatizo mengine mmeanza kuyashughulikia endeleeni lakini niwahusie kuwa zile kompyuta ni kwa ajili ya matumizi ya kazi za Serikali zisitoke kwenda sehemu yoyote fanyeni kazi kwani nasi tunafarijika kuona mnafanya kazi na kutupunguzia mzigo.’’Aliendelea kusema Bi. Zainab Telack Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa pia aliwataka Maafisa Tarafa hao kuwasimamia watendaji wa kata ili waeze kutatua migogoro inayowakabili wananchi akiongeza kuwa lengo la Serikali ni kuona wananchi wa Shinyanga wakiishi kwa furaha na amani na kutambua uwepo wa viongozi wao.
Bi. Telack amewataka Maafisa Tarafa kutunza pikipiki hizo kutokana na uwepo wa mahitaji makubwa ya pikipiki katika jamii nakuwazuia wasisimame nazo katika mabaa na kuonya kuwa Afisa yoyote atakayesema kuwa Pikipiki yake imeibiwa hataeleweka.
Wakati huo huo Afisa Tarafa Bw. Cleophasi Mdui amempongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kutekeleza ahadi yake ya kuwapatia vitendea kazi maafisa hao baada ya kuwaita Ikulu Juni 4, mwaka jana na kuhaidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kulipa fadhila kwa kiongozi Mkuu wa Nchi.
Naye Afisa Tarafa kutoka Old Shinyanga Bi. Neema Mkandala amesema usafiri huo utawawezesha Mafisa Tarafa hao kutatua kero za wananch kwa haraka ikiwemo kufika maeneo yenye shida na kutoa maelekezo kwa wananchi kwa lengo la kuboresha ufanisi.
Pikipiki hizo zimetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais John Pombe Magufuli kama kutimiza ahadi yake kwa Maafisa hao aliyoitoa tarehe 4 Juni mwaka jana Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack akiongea na vyombo vya habari pamoja na Maafisa Tarafa
wa Mkoa wa Shinyanga mapema leo Ofisini kwake Mjini Shinyanga wakati wakuwakabidhi pikipiki 14 maafisa
hao zilizotolewa na Rais John Pombe Magufuli kwa lengo la kuboresha utendaji wao.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa